.

.

.

.

Friday, March 23, 2012

MH.SEIF SHARIF HAMAD ATEMBELEA MASJID ASWABIRINA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiongozana na viongozi mbali mbali wa dini ya Kiislam alipotembelea ujenzi wa Masjid Aswabirina katika mtaa wa Kitunda Mzinga Dar es Salaam. Kushotoni kwake ni Amiri Mkuu wa taasisi za kiislamu nchini Sheikh Mussa Kundecha na kuliani ni Kadhi wa Kariakoo Sheikh Ally Basaleh.Picha na Salmin Said-Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar --- Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema jamii inahitaji vijana waliojengeka kifikra na maadili mema, hivyo kuna haja kwa vijana kuweka mkazo katika kutafuta elimu yenye manufaa kwao na jamii kwa jumla. Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika mtaa wa Kitunda Mzinga Dar es Salaam, alipokuwa akizindua harambee ya kuchangia ujenzi wa Masjid Aswabirina katika mtaa huo. Amesema msikiti ni kituo muhimu cha kutoa elimu kwa jamii na kuijenga kimaadili, hivyo ametoa wito kwa waislamu kuchangia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati. Amewashukuru wakaazi wa eneo hilo kwa kuanzisha ujenzi huo ambao utasaidia maendeleo ya dini ya kiislamu. Kabla ya uzinduzi huo, Makamu wa Kwanza wa Rais alitembelea skuli ya sekondari ya LILASIA katika mtaa huo ambako alielezwa maendeleo na changamoto zinazoikabili skuli hiyo iliyoanzishwa miaka michache iliyopita. Maalim Seif ameahidi kuchangia shilingi milioni mbili (mil. 2) kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo, na shilingi milioni moja (mil.1) kwa ajili ya skuli hiyo, sambamba na kukubali kuwa mshauri na mlezi wa msikiti huo. Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Kadhi wa Kariakoo jijini Dar es Salaam Sheikh Ally Basaleh, amewataka waislamu kuacha tabia ya kuiga na kufanya ibada kwa kufuata mkumbo, na badala yake watafute elimu ili kutekeleza ibada zao kwa uhakika. Amiri Mkuu wa kijiji hicho cha Kitunda Mzinga sheikh Khatib Yunus amesema wanakusudia kuufanya msikiti huo kuwa kituo cha taaluma na misaada kwa jamii, ambapo wanakusudia kuwasaidia mayatima 41, wajane 9 na wazee wasiojiweza katika kijiji hicho, sambamba na kuanzisha madrasa kwa ajili ya akinamama. Kiasi cha shilingi milioni mia mbili zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi milioni nne na nusu zimeshatumika. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini ya kiislam akiwemo Amiri Mkuu wa taasisi za kiislamu nchini Sheikh Mussa Kundecha. Na Hasssan Hamad Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar

No comments:

Post a Comment