.

.

.

.

Wednesday, April 18, 2012

HONGERA SHYROSE BHANJI

Mwandishi wa habari mwandamizi wa siku nyingi, Shyrose Bhanji amekuwa miongoni mwa wagombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki ambao waliibuka kidedea katika uchaguzi uliofanyika jana mjini Dodoma.

Katika uchaguzi huo wagombea tisa kati ya 32 waliowania nafasi hiyo, walifamikiwa kuibuka kidedea na kupata tiketi ya kuwakilisha Tanzania katika bunge hilo.

Wagombea walioshinda nafasi kwa wanaume Tanzania Bara na idadi ya kura kwenye mabano ni Adam Kimbisa (210), Benard Murunya (135) na Makongoro Nyerere (123), na walioanguka ni Lifa Chipaka (8), William Melecela (42), Dk. Evans Rweikiza.

Upande wa wanawake, walioshinda ni Angela Kizigha (166), Shyrose Bhanji (120), ambao ndiyo watakaiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, na walioshindwa ni Janeth Mbene, Fancy Nkuhi, Janeth Mmari na Dk. Godbertha Kinyondo.

Kundi la wagombea kutoka Zanzibar, walioshinda ni Abdalah Ali Mwinyi (237), Maria Yahya Ussi (91). Walioanguka ni Ahmada Hamad Khatib, Dk. Haji Mwita Haji, Khamis Jabir Makame, Dk. Said Gharib Bilal na Zubeir Ali Maulid.

Kwa upande wa kundi la upinzani, walioshinda ni Nderakindo Kessy (NCCR-Mageuzi) na Twaha Issa Taslima (CUF). Mgombea wa CHADEMA Antony Komu aliangushwa vibaya kwenye kinyang’anyiro hicho. Wengine walioshindwa ni Dk. Fortunatus Masha (UDP), Anthony Komu (CHADEMA), Juju Danda (NCCR-MAGEUZI), Michael Mrindoko (TLP), Mwaiseje Polisya (NCCR-MAGEUZI).

Wabunge wa CHADEMA ambao awali walitangaza kususia uchaguzi huo, walishiriki ikiwa ni pamoja na kusimamisha mgombea wake Anton Komu, ambaye alibwagwa vibaya.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe, alisema hawatashiriki uchaguzi kwa madai ya kutokuwa huru na haki.

Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, alisema wabunge wa chama hicho watatoka nje na hawatakuwa tayari kuwasikiliza wagombea wala kupiga kura na kwamba CHADEMA kushiriki uchaguzi huo ni kutowatendea haki Watanzania, lakini katika hali ya kushangaza wabunge hao wakiongozwa na Mbowe walishiriki uchaguzi huo na hawakutoka ukumbini.

Awali, CHADEMA lilitaka kupewa nafasi moja kwa ajili ya chama hicho pekee badala ya kushindaniwa na wapinzani wote kama kanuni inavyoelekeza.

‘Sisi kama Chadema hatutashiriki katika uchaguzi huo wala hatutashiriki kupiga kura wala kusikiliza tutatoka nje tuache waendelee,’ alisema.

Hata hivyo, Naibu Spika Job Ndugai, alisema hoja hiyo ya CHADEMA haina msingi na kwamba, nafasi mbili walizopewa wapinzani zitahusisha vyama vyote vya upinzani. 

Awali, wagombea waliingia katika nafasi hiyo ni Bernard Murunya, Adam Kimbisa, Makongoro Nyerere, Mrisho Gambo, Siraju Kaboyonga, William Malecela, Dk. Evans Rweikiza, Elibariki Kingu na Dk. Edmund Mndolwa wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM). Pia, yumo John Lifa-Chipaka wa TADEA.

Kwa upande wa wanawake mchuano kuwania nafasi hiyo ulikuwa kwa Engela Kizigha, Fancy Nkuhi, Dk. Godbertha Kinyondo, Janet Mmari, Janeth Mbene, Mariam Ussi Yahya na Sebtuu Mohamed Nassor, Shyrose Bhanji, Sofia Ali Rijaal wote kutoka CCM wakati mgombea kutoka upinzani ni Rose Mwalusamba (CUF).

Waliowania nafasi ya kuwakilisha Zanzibar katika Bunge la Afrika Mashariki walikuwa ni Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Dk. Ahmada Hamad Khatib, Dk. Haji Mwita Haji, Khamis Jabir Makame, Dk. Said Gharib Bilal na Zubeir Ali Maulid wote kutoka CCM.


Kwa upande wa wagombea wa vyama vya upinzani, walikuwemo Dk. Fortunatus Masha (UDP), Anthony Komu (CHADEMA), Juju Danda (NCCR-MAGEUZI), Micah Mrindoko (TLP), Mwaiseje Polisya (NCCR-MAGEUZI), Nderakindo Kessy na Twaha Issa Taslima (CUF).

Adamu Kimbisa


Angela Kizigha


Makongoro Nyerere(picha na habari kwa hisani Nkoromo Daily Blog)

No comments:

Post a Comment