.

.

.

.

Thursday, April 12, 2012

ZIMWI LA BALAA LAZIDI KUIANDAMA ATCL

KUANGUKA kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma kumeliacha  shirika hilo likiwa halina ndege hata moja inayofanya kazi, kwani ndege yake nyingine imekuwa katika matengenezo kwa muda mrefu sasa.
    
Hali hiyo bila shaka itakuwa imeifanya Serikali iukubali ukweli mchungu kwamba ATCL haikidhi tena vigezo vya kuwa shirika la ndege. Hivyo, tunadhani itakuwa imeona kwamba wakati sasa umefika wa kuacha porojo na kuanzisha shirika la ndege imara litakaloingia katika biashara ya ushindani na kupeperusha vizuri bendera ya Tanzania katika anga za kimataifa.
   
Shirika hilo lilisema juzi kwamba ndege hiyo haifai tena kubeba abiria kutokana na kuharibika vibaya na kwamba halitatoa huduma  za usafiri hadi hapo litakapopata ndege nyingine. Lakini katika hali ya kuonyesha kwamba moja ya matatizo yanayolikwaza shirika hilo ni ukosefu wa weledi kwa upande wa uongozi ni pale Kaimu Mtendaji wa shirika hilo, Paul Chizi aliposema juzi kwamba shirika hilo haliwezi kufa kwa kuwa lina mipango mingi ya kuhakikisha linafufuka.
   
Ni kweli kama alivyosema mkurugenzi huyo, ajali hiyo ya ndege hiyo ya ATCL  imelisababishia shirika hilo hasara kubwa hata kama ilikuwa imekatiwa bima, kwani shirika hilo litalazimika kukodi ndege nyingine ili kuwasafirisha abiria ambao tayari walikuwa wamekata tiketi za kusafiri katika sehemu mbalimbali nchini. Jambo linalotupa wasiwasi ni pale tunapohisi kwamba shirika hilo linayachukulia kirahisi matatizo yanayolisibu hivi sasa kiasi cha kudhani kwamba, iwe isiwe litaendelea kuwapo.
   
Ndiyo maana hatuelewi wapi Kaimu Mkurugenzi huyo, Paul Chizi alikopata ujasiri alipowaambia waandishi wa habari juzi kwamba, shirika hilo linatarajia kupata mshirika wa kibiashara atakayekuwa anatoa huduma katika mikoa ya Mwanza na Kigoma. Tunasema hatujui alikopata ujasiri huo kwa sababu tukitilia maanani hali mbaya shirika hilo liliyomo, ni mwendawazimu pekee anayeweza kuwekeza au kujihusisha na shirika hilo kibiashara.
   
Tuliwahi kuonya kwamba ATCL haiwezi kuboresha huduma zake kwa wateja na kushindana katika soko la biashara  hiyo ya usafiri wa anga kwa kauli za kisiasa kama anazotoa mkurugenzi huyo. Wakati alipoteuliwa kukaimu nafasi hiyo yapata mwaka mmoja uliopita, alitoa kauli zilizotafsiriwa kama kujipigia  chapuo kwa lengo la kulinda ajira yake na wenzake, pale alipochukua muda mwingi kuishukuru Serikali kwa kufufua shirika hilo na kutoa ahadi tele kwamba  shirika hilo lingefanya miujiza na maajabu, huku akijua kwamba shirika hilo halikuwa na nyenzo, mitaji  wala rasilimali za kuliwezesha kutoa huduma kwa ufanisi.
   
Tulisema shirika hilo lisingeweza kufanya miujiza pasipo kupewa mtaji wa kutosha na pasipo kuwa na ndege zenye ubora, marubani na wahandisi wenye weledi na uzoefu wa kuliwezesha shirika hilo kuweka mazingira ya kushindana kibiashara. Tulisema pia Serikali ilipaswa kutoa dhamana ili liweze kupata mikopo ya kibenki. Mbona majuzi Serikali hiyohiyo iliidhamini Tanesco ili ipate mkopo wa Sh408 bilioni kutoka benki moja ya kigeni hapa nchini?
   
Tumesema hapo juu kwamba Serikali pengine itakuwa imeng’amua kwamba wakati wa maneno mengi na porojo umekwisha katika suala la uanzishwaji wa shirika la ndege lenye sifa na uwezo wa kupeperusha bendera ya nchi yetu kutokana na ukweli kwamba, ATCL ilianzishwa kuirithi ATC pasipo kuwapo dhamira, mipango na mikakati madhubuti ya kuingia katika soko la biashara ya ushindani ya usafiri wa anga. 
   
Sasa tunaambiwa kuwa, Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athuman Mfutakamba imelipa mamlaka shirika hilo mamlaka ya kukodi ndege kutoka mahali popote ili kuziba pengo lililoachwa na ndege ya shirika hilo iliyoanguka Kigoma juzi. Sisi tunadhani huko ni kukwepa tatizo, kwani ATCL  ilivyo sasa haifufuliki. Serikali ijitose kwa kuanzisha shirika jipya na kulipatia mitaji ya kupata ndege za kutosha, watendaji wenye weledi na marubani na wahandisi wa ndege wenye uzoefu mkubwa.

No comments:

Post a Comment