.

.

.

.

Friday, May 11, 2012

TALAKA ZAZIDI ZANZIBAR

KADHI Mkuu wa Mahakama ya Kadhi Wilaya ya Kati Unguja, Shehe Ali Zubeir Mohammed amesema kumejitokeza wimbi la utoaji wa talaka kwa wanaume usiozingatia maadili na kwa mwaka jana pekee, zaidi ya talaka 19 zimetolewa. 

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mwera Wilaya ya Kati Unguja, Shehe Zubeir alisema wanaume wamekuwa wakitoa talaka bila ya kuzingatia maadili na sheria zinazoongoza ndoa na dini ya Kiislamu na hivyo kusababisha matatizo makubwa ikiwemo kusambaratika kwa familia ikiwamo watoto. 

Alisema Mahakama ya Kadhi ya Mwera kwa asilimia 70 inapokea kesi zinazohusu mambo ya talaka huku wanawake wakilalamika kutaka kupewa talaka baada ya kuchoshwa na vitimbi vya wanaume. 

“Kesi za matukio ya madai ya talaka ndiyo zinazoongoza katika Mahakama ya Kadhi kwa sasa. Si katika Mahakama ya Mwera tu, hata Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,” alisema Shehe Zubeir ambaye kabla ya uteuzi wa kuja Mwera, alikuwa akifanya kazi katika Mahakama ya Mwanakwerekwe mjini Unguja. 

Alisema kutokana na kuibuka kwa madai ya kesi za talaka, tatizo la kutelekezwa kwa familia ikiwamo watoto hujitokeza kwa kasi. Alisema kwa mwaka jana, zaidi ya kesi za madai ya kutelekezwa familia 10 zimeripotiwa katika Mahakama ya Kadhi Mwera. 

“Tunapokea kesi za wanaume kutelekeza watoto wao ambapo tunazipatia ufumbuzi kwa kupeleka barua kazini kwao na kutaka kukatwa katika mishahara yao kwa ajili ya kuhudumia familia,” alisema na kuongeza kuwa zaidi ya kesi tano zimetolewa hukumu kwa wanaume kukatwa katika mishahara yao ili kuhudumia familia. 

Shekh Zubeir aliitaka Serikali kuimarisha huduma za Mahakama ya Kadhi kwa kuipa hadhi kamili sawa na mahakama za kawaida kwa sababu majukumu yake ya kuhudumia wananchi ni makubwa. 

Utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), umegundua Mahakama za Kadhi zimetupwa na Serikali licha ya kupewa majukumu makubwa ya kutoa hukumu na kuipatia ufumbuzi migogoro na kesi katika ngazi za familia. 

Kwa mfano, katika Mahakama ya Mwera na Mwanakwerekwe, kesi zinaendeshwa bila ya kuwapo kwa vyombo vya ulinzi ikiwamo Polisi, tofauti na Mahakama za kawaida na hivyo kusababisha wakati mwingine utekelezaji wa amri kutozingatiwa au kutekelezwa. 

“Hizi Mahakama za Kadhi zimedharauliwa licha ya kuundwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar katika Ibara 150 zinataja kuwapo kwa Mahakama ya Kadhi katika Sheria Namba 3 ya mwaka 1985 na kufanyiwa marekebisho yake katika mwaka 2002,” alisema wakili wa kujitegemea anayefanya kazi zake katika Mahakama ya Kadhi, Ali Omari. 

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu wakati alipofanya ziara kukagua Mahakama za Mkoa pamoja na Mahakama za Kadhi, alisema Serikali inakusudia kuzipa uwezo zaidi Mahakama za Kadhi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake kikamilifu. 

Mahakama za Kadhi zipo kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Zanzibar, na moja ya kazi yake kubwa ni kushughulikia migogoro na matatizo yanayoihusu jamii ya Waislamu ikiwamo ya ndoa, talaka na urithi na kutoa hukumu zake.

1 comment: