.

.

.

.

Friday, May 11, 2012

WANAWAKE 4 WAUWAWA KINYAMA


Wanawake wanne wameuawa kwa mpigo baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kutokana na imani za kishirikina katika Kijiji cha Luezela Kata ya Nzera  wilayani Geita.
Tukio hilo lilikuja baada ya mtoto mwenye umri wa miaka mitano, Diana Salu, kuuawa kwa kutafunwa na fisi na hivyo wanakijiji kulihusisha na imani za kishirikina.
Wakazi hao pia waliteketeza kwa moto nyumba za wanawake hao.
Wakati  wanafanya mauaji hayo ya kikatili, polisi walifika eneo la tukio na  kumuokoa kikongwe mmoja anayedaiwa ndiye aliyekuwa mtuhumiwa mkubwa.
Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa na vyanzo mbalimbali zimedai kuwa mtoto Diana alikamatwa na kutafunwa na fisi juzi saa 1:30 usiku katika Kijiji cha Luezela, alipokuwa akirudi kutoka dukani kununua biskuti.
Imeelezwa kuwa baada ya mtoto huyo kukamatwa na fisi huyo, alipiga kelele kuomba msaada, lakini wanakijiji walipokwenda eneo la tukio, walikuta tayari amekwisha kutafunwa baadhi ya viungo ukiwemo mguu na sehemu za siri.
Kwa mujibu wa habari hizo, wanakijiji hao walianza kumfukuza fisi huyo kwa lengo la kumuua.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa fisi huyo alipotea kitatanishi baada ya kufika jirani na nyumba ya mmoja wa watuhumiwa waliouawa.

Imeelezwa kwamba baada ya wanakijiji kuona hivyo, walihamasishana na kuingia ndani ya kikongwe huyo, Lolensia Bagili (70), mkazi wa kijiji hicho na kisha kumtaka awaonyesha fisi huyo alikokwenda.
Habari zinasema kuwa kikongwe huyo aliwajibu kwamba fisi huyo alikuwa katika nyumba ya mwezao kisha walimwamuru awapeleke na walipofika walikuta hayupo na ndipo walipoanza kumpiga kwa marungu na mapanga hadi walipomuua papo hapo.
Baada ya kumuua, wanakijiji hao walikwenda kuteketeza kwa moto nyumba yake.
Aidha, imedaiwa kuwa walipokuwa wakimpiga kikongwe huyo, walimtaka awataje wenzake anaofanya nao uchawi na inadaiwa kuwa aliwataja wengine wanne ambao kati yao ni mmoja tu aliyenusurika kuuawa na wanakijiji hao baada ya kujificha katika uvungu wa kitanda katika nyumba ya mtoto wake wa kike hadi polisi walipofika eneo hilo na kumnusuru.
Kadhalika, wanakijiji hao walikwenda nyumbani kwa Kulwa Mashana (55), Roze Mabeshi (60) na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Mwanakonya, na kuwashambulia mmoja baada ya mwinginne hadi kufa.
Baada ya kuwaua, wanakijiji hao walichoma moto nyumba zao na kuteketeza kila kilichowemo ndani yake.
Miili ya marehemu hao ilikuwa inasubiri kufanyiwa uchunguzi kabla ya mazishi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Philemon Shelutete, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa alikuwa njiani kuelekea eneo la tukio.
“Ni kweli Bwana Mwandishi hadi ninapozungumza na wewe, tayari watu wanne nimethibitishiwa na Polisi wameuawa katika tukio hilo linalodaiwa chanzo chake ni mtoto wa kike kuliwa na fisi katika kijiji cha Luezela.
Ninaelekea huko eneo la tukio kwa sasa sijafahamu kama wapo waliokamatwa au bado, lakini hali ya utulivu imerejea,” alisema Shelutete.
Aidha, polisi walipelekwa eneo la tukio kurejesha hali ya utulivu na amani.
Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa wanaume wa kijiji hicho wamekimbia na kwenda porini kujificha wakihofia mkono wa sheria kutokana na polisi kupelekwa kukabiliana na vurugu hizo.
Imani za kishirikina katika maeneo kadhaa ya Kanda ya Ziwa  zimekuwa zikisababisha mauaji ya watu wasio na hatia kutokana na watu kuamua kujichukulia sheria mikononi.

MAMA ADAIWA KUUA  MWANAYE, KUMFUKIA SHIMONI

Jeshi la Polisi linamshikilia mwanamke mkazi wa kitongoji cha Sirari, wilayani Tarime, Mkoa wa Mara  Mwadawa Joseph (18), kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mwenye umri wa miezi mitatu kwa kumfunga kwa kamba mikono na miguu kisha akamfukia shimoni.

Mwanamke huyo anadaiwa kufanya mauaji hayo ya kikatili dhidi ya mtoto huyo, Naomi Marco, kwa kile kilichodaiwa ni kutokana na mzazi mwenziye kutotoa matunzo kwa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kamanda Kamugisha alisema mwanamke huyo inadaiwa alizaa na kijana mmoja aliyetajwa kwa jina la Marco, lakini alikuwa hampi mtoto matunzo, jambo lililomfanya afikie hatua ya kumuondoa duniani ili kuondokana na adha hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, tukio la kuuawa kwa mtoto huyo lilitokea Mei 8, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema majirani wa mwanamke huyo waliingiwa na wasiwasi baada ya kumuona ghafla hana mtoto kwa siku mbili mfululizo na hivyo wakatoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sokoni, Robert Nashon.

Kamanda Kamugisha alisema uongozi wa kijiji pamoja na wananchi walifanya msako na kubaini mtoto huyo alipozikwa.
Alisema walimkamata mtuhumiwa huyo na kumhoji na ndipo alipokwenda kuwaonyesha mahali alipomzika mtoto huyo.
Aidha, alisema wananchi kwa kushirikiana na Polisi walifukua shimo alilokuwa amefukiwa mtoto huyo lenye kina cha futi tatu na kukuta maiti yake ikiwa imefungwa kamba miguuni na mikononi.
Hali hiyo iliwatia wananchi hasira wakihisi kuwa huenda mtoto huyo alizikwa akiwa hai na kutaka kumshambulia mwanamke huyo kwa mawe. Hata hivyo, aliokolewa na Polisi wa Kituo cha Sirari.
Alisema polisi wanaendelea kumhoji mwanamke huyo huku wapangaji wenzake wawili aliokuwa akiishi naye nyumba moja wanadaiwa kukimbia mji huo baada ya ya mauaji hayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment