.

.

.

.

Wednesday, July 03, 2013

ALICHOSEMA MAGGID MJENGWA JUU YA VYAMA VYA SIASA NCHINI

Ndugu zangu,

Katika saa 20 na zaidi Rais Obama alipokuwa katika ardhi ya Tanzania, sikusikia mahali popote akitamka jina la chama chake cha Democrat. Obama ametamka ' AMERICA!' mara zisizohesabika.

Kwa kweli ujio wa Obama umetusaidia Watanzania kupumzika na kelele za vyama, maana, kwa siku kadhaa, kabla na wakati wa ujio wa Obama, Watanzania tumepata kupumzika na kusikia habari za
vyama vya siasa na malumbano yasio na hoja za msingi, mara nyingi yasio na tija kwa nchi na maendeleo yake.

Hakika, siasa ni kitu kizuri sana kwa nchi. Lakini siasa za ' ovyo ovyo' ni kitu kibaya kwa nchi. Na mara nyingi, siasa za ' ovyo ovyo' ni kitu cha hatari kwa nchi na mustakabali wake.

Picha hiyo hapo juu ina mengi ya kutufundisha; kuwa siasa si uhasama. Uchaguzi ukiisha watu mnarudi kwenye kufanya kazi. Kupigania maslahi ya taifa. Si kuendeleza migogoro ya kisiasa na hata kuwepo kwa vurugu. Hayo hayana tija kwa nchi.

Unapomwangalia Obama na Bush kwenye picha ya pamoja wakiwa Dar na kwenye kutoa heshima kwa wahanga wa ugaidi kwenye mlipuko ulitokea kwenye Ubalozi wao mwaka 1998, inadhihirisha ukomavu wa kisiasa.

Unachotumainia hapa, kuwa ifike siku, hata hapa kwetu Tanzania, kwa Rais aliye madarakani na Rais Mstaafu kutoka vyama viwili tofauti, tuone picha yao wakiwa wamesimama pamoja kwenye makaburi ya kumbukumbu ya mashujaa wetu wa Vita Vya Kagera kule Uganda.

Ndio, picha hiyo hapo juu ni somo kwetu. Hawa wawili; Bush na Obama, ndio tuliowaona kwenye kampeni zao wakipambana kiasi huwezi kufikiri wanaweza kusimama pamoja kama ndugu wa taifa moja.

Lakini, kwa wenzetu Marekani, siasa si uhasama wala mambo ya kuwindana. Wanachogombania kwenye siasa ni kupewa heshima ya kuitumikia Marekani.

Na heshima hiyo akipata mpinzani wako, basi, kwa wenzetu wanachofanya ni kuungana mkono kwenye kazi ya maslahi ya Marekani bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Na ndicho tunachofundishwa kwenye picha hiyo.

Swali linabaki, Watanzania tuko tayari kubadilika kifikra kwa maslahi ya taifa letu?

Maggid,
Iringa.
0754 678 252

No comments:

Post a Comment