.

.

.

.

Tuesday, September 17, 2013

LIGI YA KLABU BINGWA ZA ULAYA UEFA YAANZA KWA KISHINDO

KIPENGA cha Ligi ya Mabingwa ya UEFA kilipoanzwa kupulizwa majira ya saa 1.45 usiku huu katika viwanja nane tofauti barani Ulaya, pengine mashabiki wa kandanda kote ulimwenguni hawakuwa na matarajio ya matokeo ya namna hii.
Katika dimba la Old Trafford wakati Manchester United wakimenyana vikali na Bayer Leverkusen, ni Wayne Rooney aliyewadhihirishia mashabiki wa klabu hiyo kuwa yeye yungali mtumishi wao mwaminifu baada ya kutia kimiani magoli mawili muhimu mno kwa Mashetani Wekundu wa Old Trafford.  Rooney alifunga mabao hayo katika dakika ya 22 na 70.  Mpachika mabao namba moja Robin van Persie lifunga bao la aina yake la tik tak panapo dakika ya 59 huku Luis Antonio Valencia akifanya hivyo dakika ya 79.  Magoli ya Bayer 04 yakatiwa wavuni katika dakika ya 54 na 88.
Matokeo mengine ya kusisimua zaidi yalikuwepo jijini Instabul nchini Uturuki wakati wenyeji Galatasaray wamepata aibu ya mwaka baada ya kugaragazwa na Real Madrid kwa mabao 6-1 huku Cristiano Ronaldo akifunga hat-trick.  Naye Karim Benzema hakuwa na hiyana pale alipotupia wavuni magoli mawili huku Isco akiwa wa kwanza kufungua karamu hiyo panapo dakika ya 33.
Matokeo mengine yenye karamu ya magoli ni pale wamwaga fedha wakubwa Paris Saint-Germain walipoitandika bila huruma Olympiacos tena katika uwanja wao wa nyumbani magoli 4-1.  Mechi hiyo iliyokuwa ya vuta n'kuvute ya aina yake imewashuhudia Wagiriki hao wakishindwa kutamba katika dimba lao la nyumbani na kuwaruhusu PSG kuzuru langoni kwao mithili ya lango la sokoni uingiapo kila unapojisikia.  Ni Thiago Motta aliyetia wavuni magoli mawili katika dakika ya 68 na dakika tano baadaye akafunga goli jingine baada ya Edinson Cavan kufungulia sherehe hiyo huku Olympiacos wakifunga dakia ya 25 kupitia kwa Vladimir Weiss.  Mkali Zlatan Ibrahimovic alikosa penati dakika ya 82 baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa wa Olympiaco.  Akawa Marquinos panapo dakika ya 86 akiifungia PSG goli la nne.
Mabingwa watetezi, Bayern Munich imewatandika CSKA Moscow magoli 3-0 huku ikutumia vema uwanja wake wa nyumbani.  Magoli ya Bayern Munich yamefungwa na David Alaba dakika ya 4, Mario Mandzukic dakika ya 41 na Arjen Robben katika dakika ya 68.
Matajiri kutoka Uingereza, Manchester City wameonesha ubabe wao ugenini baada ya kuwatandika bila huruma Victoria Plzen magoli 3-0 yaliyotiwa wavuni na Edin Dzeko dakika ya 48, Yaya Toure dakika ya 53, na Sergio Aguero panapo dakika ya 58.
Shaktar Donetsk akiwa ugenini amemtwanga Real Sociedad magoli 2-0 yaliyotiwa wavuni na Alex Teixeira katika katika ya 65 na 87.  Nao Benfica wameutumia vema uwanja wao wa nyumbani baada ya kuwafunga Anderlecht magoli 2-0.  Magoli hayo yalitiwa kimiani na Filip Djuricic dakika ya 4 na Luisao dakika ya 30.
Juventus wakiwa ugenini wametoshana nguvu na FC Kobenhavn baada ya kwenda sare ya 1-1.  Wenyeji ndiyo walioanza kupata bao dakika ya 14 kupitia kwa Nicolai Jorgensen.  Juventus wakasawazisha dakika ya 54 kupitia kwa Fabio Quagliarella.
Siku ya Jumatano kutakuwa na mechi za makundi E, F, G na H.  Mechi zitakuwa kama ifuatavyo:
Chelsea vs Basel
Schalke 04 v Steaua Bucuresti
KUNDI F
Marseille v Arsenal
SSC Napoli v Borussia Dortmund
KUNDI G
Atletico Madrid v Zenit Petersburg
Austria Wien v FC Porto
KUNDI H
AC Milan v Celtic
Barcelona v Ajax
Mechi zote zitachezwa saa 3.45 kwa saa za Afrika Mashariki

No comments:

Post a Comment