WIKI hii iliyopita imekuwa na mijadala mingi kuhusu mtu aliyeiaga dunia miaka 14 iliyopita lakini, pamoja na kuwa ni marehemu, amebakia kuonekana kama kiongozi wa kweli wa watu wake.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amekuwa na mvuto usiokuwa wa kawaida miongoni mwa Watanzania wa rika zote, na hata miongoni mwa watu wa nje ya nchi hii waliomjua binafsi na waliomsoma na kum-google.
Katika kuadhimisha maisha yake, watu wengi wamejaribu kufanya tathmini ya kile ambacho hasa kinamfanya mzee huyu aliyelala kijijini kwake Butiama aendelee kuwa na ushawishi mkubwa kiasi hicho, na kila aliyetoa maoni yake amekuwa na lake la kusema.
Nimesoma mahali kadhaa, na pia nimesikia kwenye mijadala ya redio, watu wakistaajabu kutokana na uwezo wa mtu aliyefariki muda wote huu kuwa anaendelea kuiongoza nchi kutoka kaburini.
Hatuna sababu ya kustaajabu kuhusu hili. Ingawaje haiwatokei binadamu wengi, lakini si ajabu kwa mtu aliyeishi maisha ya aina fulani kuendelea kuwa na ushawishi mkubwa hata baada ya kifo chake. Hii imetokea mara nyingi pale wanapoondoka watu waliofanya mambo makubwa wakati wa maisha yao, na hususan wale waliotenda mema.
Kwa hakika, hivyo ndivyo wanavyokuwa watu walioanzisha imani za kiroho zilizovuta hisia za wafuasi wengi, na imani hizo zikazidi kukua, kusambaa na kutangaa hadi zikafika sehemu ambazo waanzilishi wake hawakujua kwamba zipo sehemu za aina hiyo. Ndivyo ilivyo kwa imani za dini zilizotoka Mashariki ya Kati na hivi sasa zimetandaa ulimwenguni kote.
Viongozi wa kisiasa pia wanaweza kuwa na ushawishi kama huo wakiwa wamelala kaburini, na wakati mwingine wafuasi wao waliowarithi hujaribu kuwatumia ili wapate kukubalika mbele ya halaiki. Nahisi hiki ndicho chanzo cha kuwajengea makaburi ya aina ya makumbusho (mausoleum) na kuifanya miili yao ionekane kama wamelala tu, hawakufa.
Nyerere amezikwa Butiama, kama ilivyo ada ya imani yake ya kidini, lakini jina lake limeanza kuwa na ladha ya kinabii, kama vile alianzisha imani ya kidini ambayo wafuasi wake wanataka kuinedeleza na kuieneza kote wawezako kufika.
Nimesema hapo juu kwamba hata nje ya nchi wako wafuasi wa Nyerere wanaochukua sura ya waumini wake. Jaji Mkuu wa Kenya, Dk. Willy Mutunga amenukuliwa akisema kwamba yeye ni “mwathirika wa virusi vya Azimio la Arusha” na kwamba ni muumini wa sera za Nyerere. Si tofauti sana na imani za kidini, na wako wengi wa aina hii.
Inawezekana kwamba hali hii inasababishwa na ukame wa viongozi tulionao, si hapa nchini kwetu tu, bali katika bara la Afrika na duniani kote. Inawezekana ni kutokana na ‘nostalgia’, kw amaana ya kukumbuka kwa kujutia siku za nyuma na kuziona kama zilikuwa bora kuliko hizi tulizo nazo. Lakini inawezekana kuna jambo jingine.
Nimewahi kuandika mara kadhaa kwamba Nyerere hakuwa malaika, na kwamba alitenda makosa mengi katika kuiongoza na kuitawala nchi hii. Yumkin, hilo ndilo linatuthibitishia kwamba kwa hakika alikuwa binadamu, la sivyo tungemwita muungu.
Tofauti kati yake na wengine ni kwamba alitenda makosa aliyoyatenda katika jitihada za kuiendeleza nchi yake na kuwainua wananchi wake kutoka katika masikini na unyonge. Hakutenda makosa yaliyotokana na utashi wa kujitajirisha yeye na familia yake wala kwa nia ya kusimamia maslahi ya mitaji mikubwa ya “wawekezaji” na waporaji kutoka nje.
Aliishi maisha ya mtu wa kawaida; alipenda kuvaa kama mtu wa kawaida; alichukia anasa na tabia za kujipamba mithili ya tausi; magari yake yalikuwa si yake bali ya dola, na yalikuwa magari ya kawaida kabisa; alichukia mbwembwe zisizo na maudhui. Alipenda kufanya kazi, wakati mwingine kazi za ngwamba ambazo watu wengi huzikimbia.
Misimamo yake ilikuwa imara na isiyoyumba, na ndiyo maana wawakilishi wake nje ya nchi waliweza kutoa matamko yalaiyofanana bila kuwasiliana juu ya wanachokisema, kwani bosi wao alikuwa anaeleweka. Na tusisahau kwamba hii ilikuwa ni katikati ya malumbano makali kuhusu mapambano ya ukombozi wa Afrika, na diplomasia yetu ilibidi ipambane na diplomasia ya kinafiki ya nchi za Mgharibi maswahiba wa makaburu.
Nakumbuka nilipokuwa naanza kazi kama mwanahabari jijini, nikiwa na mijadala isiyoisha na mwanahabari mwandamizi, tulikua tukijiuliza iwapo baada ya Mwalimu tungeweza kumpata mtu wa kumrithi. Tuliona kwamba ingekuwa vigumu kumpata mtu ambaye angekubali majukumu mazito kama hayo.
Muonekano wa kazi ya kuongoza nchi wakati ule ulikuwa muonekano wa majukumu matupu, si raha. Nani angekubali kuishi vijijini na Wagogo na Waha kwa mwezi mzima, na kuamka kila siku saa 11 alfajiri kwenda kushinda analima kwa jembe la mkono?
Nani angekubali kila siku kuwa katika kampeni vijijini na mijini kuhimiza kisomo cha watu wazima, uzazi wa mpango, kilimo cha kisasa na kila aina ya kampmeni za ‘kipedagogia’ kwa watu wake?
Diplomasia ulikuwa ni uwanja mwingine ambako Nyerere alitoa mchango mkubwa kuisogeza Afrika mbele, hasa katika masuala ya ukombozi na kutofungamana na upande wo wote. Aidha alikuwa msitari wa mbele katika kudai mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi wa kimataifa (NIEO), na juhudi zake zinakumbukwa duniani kote.
Alikwenda mara chache sana kuhutubia Baraza Kuu la Umoja waMataifa (UNGA), lakini kila alipofanya hivyo hotuba yake ilibakia kuwa ni mpango wa kufanyiwa kazi na Umoja wa Mataifa kwa mwaka uliofuata. Alikuwa kiongozi miongoni mwa viongozi wa dunia.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment