.

.

.

.

Saturday, January 18, 2014

HARUSI YA MTOTO WA RAIS MIRAJI KIKWETE


Miraji Kikwete na Aima Mahmoud wakiondoka kwenye ukumbi wa Mlimani City baada ya kufunga ndoa yao jana. Picha na Florence Majani  


Shamra shamra na nderemo zilitawala jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City wakati Miraji Kikwete, mtoto wa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipofunga ndoa na Alma Mahmoud.
Sherehe hizo zilianza saa 7:00 mchana baada ya ndoa kufungwa na maharusi hao kuingia ukumbini hapo wakiongozana na Rais Kikwete.
Hali nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu ingawa uwanja ulikuwa umefurika magari ya polisi, viongozi na wageni waalikwa. Huku kikosi cha kudhibiti ulinzi na usalama kikiwa kimefunga mitambo ndani na nje ya ukumbi huo.
Ulinzi katika eneo hilo ulikuwa ni mkali kupita kiasi ambapo hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia ukumbini humo bila kadi maalumu, hata angeomba kwa kupiga magoti.
“Hata sisi tumetoka Bagamoyo hadi hapa tuna undugu kabisa na mkubwa (Rais Kikwete), lakini wametunyima kwa sababu hatuna kadi,” alilalamika mwanamke mmoja aliyeongozana na wanaume wawili.
Hakuna waandishi wa habari walioruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi huo, isipokuwa waandishi na wapiga picha maalumu wa Serikali ambao walipewa vitambulisho maalumu na tisheti.
Wengine walioonekana wakipiga picha ni wanafamilia ambapo watoto wa kiume wa Rais Kikwete, walionekana wakiwa na kamera huku wamevalia kanzu nadhifu.
Mfanyakazi mmoja wa Ikulu alipomwona Mwandishi wa gazeti hili, alimfuata na kumwambia kuwa sherehe hiyo ni ya kibinafsi na haruhusiwi mwandishi yeyote kufanya kitu chochote.
“Tumenyimwa kuruhusu waandishi kwenye sherehe hii, sawa wewe ni mwandishi lakini hii ni sherehe binafsi na ya kifamilia, huruhusiwi kupiga picha yeyote,” alisema mfanyakazi huyo, jina linahifadhiwa.
Hata hivyo, mwandishi alitumia mbinu kupata picha za maharusi hao pamoja na matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea ukumbini hapo.
Wageni wengi waalikwa walianza kuingia ukumbini humo majira ya mchana na wengine waliendelea kuwasili hadi saa 11 za jioni.
Miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Waziri wa Maendeleo ya Wanawake Jinsia na Watoto, Sophia Simba

No comments:

Post a Comment