.

.

.

.

Sunday, January 19, 2014

SURA MPYA BARAZA LA MAWAZIRI

RAIS Jakaya Kikwete, ametangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambalo sura mpya zimechomoza huku wengine watano wakiwekwa kando kwa sababu mbalimbali.

Sura mpya zilizochomoza ni wabunge wafuatao na majimbo yao kwenye mabano ,
Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi), Juma Nkamia (Kondoa Kusini), Jenister Mhagama (Peramiho), Godfrey Zambi (Mbozi ), Pindi Chana (Viti Maalumu), Kaika Telele (Ngorongoro ) Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini) na  Dk. Kebwe Stephen Kebwe (Serengeti).

Walioachwa kwenye baraza ni waliokuwa Naibu Waziri Viwanda na Biashara, Gregory Teu, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Goodluck Ole Medeye.

Kwa mujibu wa Mabadiliko hayo wengine walioachwa ni waliokuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Theresia Huvisa, na Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Benedict Ole Nangoro (Kiteto).

Pia katika mabadiliko hayo Naibu Mawaziri watatu wamepandishwa vyeo kuwa mawaziri kamili ambao ni  Saada Mkula Salum (Fedha), Dk. Seif Rashid (Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii) na Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii).

Akitangaza mabadiliko hayo leo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais Kikwete amefanya mabadiliko hayo kwa mujibu wa kifungu cha 55 (4) cha Katiba kinachompa mamalaka ya kufanya hivyo.

Alisema Rais amefanya mabadiliko hayo, baada ya mawaziri wanne kujiuzulu na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa kufariki dunia. Waliojiuzulu ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha(Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Dk. Mathayo David (Mifugo na Uvuvi).

Katika mabadiliko hayo Wizara ya Fedha imepata mrithi baada kifo cha Dk.William Mgimwa kilichotokea Januari mosi mwaka huu, ambapo sasa Waziri ni Saada Mkuya Salum, ambaye alikuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo.

Balozi Sefue alisema wizara hiyo itaendelea kuwa na naibu  mawaziri wawili ambapo Mwigulu Nchemba atakashughulikia sera na Adam Malima atakayeshughulikia mapato na uchumi.

Wizara ya Maliasili na Utalii, Sefue alisema aliyekuwa Naibub Waziri, Lazaro Nyalandu sasa amekuwa waziri kamili na Naibu Waziri wake ni Mahmoud Mgimwa.

Alisema Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), itaongozwa na aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Husein Mwinyi huku Mathias Chikawe akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu wake atabaki, Pereira Ame Silima.

Balozi Sefue alisema Wizara ya Maendeleo , Rais amekteua Dk. Titus Kamani kuwa Waziri na Naibu wake ni Kaika Telele.

Alisema pia Rais Kikwete amefanya mabadiliko katika Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kumeteua Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Waziri na Naibu atabakia Angellah Kairuki.

Katika mabadiliko hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itaendelea kuongozwa na Dk. Shukuru Kawamba na Naibu Waziri mpya ni  Jenista Mhagama.

Alisema kuna mabadiliko katika Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mazingira atakuwa Dk. Binilith  Mahenge na Naibu Waziri ni Ummy Mwalimu, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto.

HABARI NA BASHIR NKOROMO

No comments:

Post a Comment