.

.

.

.

Tuesday, June 03, 2014

ALIYOYASEMA RAIS M7 JUU YA BABA WA TAIFA


Na Paul Mallimbo, Kampala, UgandaRais Yoweri Museveni, amesema kiongozi bora ni yule anayefuata maagizo ya Mungu na kuwatumikia binadamu wote kwa usawa na haki. Rais Museveni aliyasema hayo (Juni mosi) wakati ibada ya kuombea mchakato wa kumfanya Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa mwenyeheri na hatimaye kutangazwa mtakatifu. 
Alisema hata kwenye maandiko matakatifu ya Biblia kuna mistari inayomtaka binadamu ampende binadamu mwenzake kama anavyojipenda yeye;“Kwenye biblia kuna sehemu inauliza kuwa utampendaje Mungu ambaye hujawahi kumuona, na ushindwe kumpenda binadamu mwenzako,” Alisema kwa sababu aliwahi kufanya kazi na mwalimu, anaweza kutoa ushahidi kwamba mwalimu alifanya yote mawili, kumtii Mungu na kuwatumikia binadamu. 
Alisema mojawapo ya sababu iliyomfanya Marehemu Papa Paulo II kutangazwa mtakatifu kuisaidia Ulaya Mashariki, ambayo wananchi wake walikuwa hawamwamini Mungu. “Marehemu Papa Paulo II alisaidia kuikomboa Ulaya Mashariki kutoka kwenye ukomunisti, wananchi walikuwa hawaamini kuna mungu, lakini kwa juhudi zake aliwafanya wamwamini na kumpenda Mungu,”alisema. 
Rais Museveni alisema anatarajia kupeleka ushahidi kwa Papa Benedict kwamba Mwalimu anasifa za kutangazwa kuwa mtakatifu kwa sababu alimtii Mungu na kuwatumikia binadamu. “Mimi nitapeleka ushahidi kwa Papa, kwamba mbali na mwalimu kumtii Mungu na kuwpenda binadamu wote, pia aliwakomboa Waafrika kutoka Ruvuma mpaka Capetown, huu ni ukweli siyo hadithi,alisisitiza Rais Museveni. 
Kufuatia hatua hiyo ya kwenda Roma kutoa ushahidi, Rais Museveni amesema katika maadhimisho ya kuombea mchakato wa Mwalimu kuwa Mtakatifu yatakayofanyika mwakani, ameahidi kuwaita maraisi wote waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere ili kuuthibitishia ulimwengu kuwa Marehemu Baba wa Taifa ameweza kuwaunganisha Waafrika. 
Alifafanua kuwa Mwalimu ametoa mchango mkubwa wa ukombozi kwa nchi za Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika Kusini, Uganda na Tanzania yenyewe. Hivyo kuja kwa viongozi hao kushiriki ibada hii itakuwa Baraka kubwa. 
 Rais Museveni ambaye alitumia muda mwingi wa hotuba yake kuzungumza Kiswahili, alisema baada ya jitihada za mwalimu kuikomboa Uganda, ndipo na wao walipoweza kuzisaidia nchi za Rwanda, Sudan Kusini na Congo kujikomboa na kuongeza kuwa kama si juhudi za mwalimu wasingekuwa na uwezo wa kuwasaidia wengine. 
Aidha Rais huyo wa Uganda ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, alisema kuwa, kwa upande wa viongozi weusi, hakuna kiongozi ambaye ametoa mchango mkubwa kama Marehemu Mwalimu Nyerere. 
“Hapa Duniani sidhani kama kuna mtu mweusi mwingine ambaye ametoa mchango kama mwalimu, na hili nimelishudia mwenyewe sikuambiwa na mtu, aliongeza kuwa, hata mzee wetu Nelson Mandela alifanya kazi kubwa Afrika ya Kusini lakini Mwalimu alifanya kazi kubwa zaidi ya ukombozi wa Afrika, Alisema. 
Alisema Mwalimu aliikomboa Tanzania na kuwafundisha dini ya Kristu, kwa vitendo siyo kwa maneno. Aliongeza kuwa nchi nyingine za Afrika zimepatwa na machafuko ya ukabila na dini kutokana na msingi mbaya wa viongozi waliotangulia. 
“Tanzania ni nchi ya Wakristo, Waislamu na wale wengine wanaoamini dini za kienyeji lakini mwalimu aliwafundisha Watanzania fikra za kizalendo za umoja,alisema . 
Alisema Uganda haikupata elimu nzuri juu ya jambo hilo, viongozi wa kwanza wa taifa hilo waliwapandikiza wananchi chuki, kwamba dini ni kumchukia mwenzako, waumini wa dini moja kuwachukkia waumini ya dini dini nyingine na matokeo yake ni umwagaji wa damu.
 “Biblia inasema kile unachopanda ndicho unachovuna, kwa hiyo sisi hapa tulipanda mbegu mbaya na tukavuna umwagaji wa damu,” alisema na kuongeza kuwa Tanzania haijawahi kuona umwagaji mkubwa wa damu zaidi ya ajali za magari na ile ya kipindi kile wakati askari wa Tanzania walipokwenda Uganda kupigana na Idd Amin.
Nadhani hii ndiyo damu pekee mmeona,” alisema. 
 Alisema baadhi ya waasisi wa Uganda waliwafundisha kuwa wakristu kuwachukia Waislamu, matokeo yake nchi imekuwa katika umwagaji wa damu tangu ilipopata uhuru. Aliongeza kuwa mpaka 1986 wakati anaingia madarakani raia 800,000 wa Uganda walikuwa wamekufa kutokana na chuki za udini na ukabila. 
“Uganda imeshuhudia umwagaji mkubwa sana wa damu, Congo wameona damu, Sudan, Somalia, Kenya, Rwanda na Burundi ni Tanzania pekee ambayo imekuwa kama kisiwa cha amani, hii yote ni kutokana na mchango wa mwalimu Nyerere ambaye alidumisha amani, umoja na maendeleo kwa watu wake.
 Alisisitiza kuwa, kwa sababu mojawapo ya sababu ya kumfanya mtu awe mtakatifu ni watu kutoa ushahidi wa matukio mbali mbali yaliyofanywa na mtu huyo wakati wa uhai wake, aliahidi kwenda Roma kutoa ushahidi kuhusu matendo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. 
“Nikienda kwa Baba Mtakatifu, Papa Benedict nitatoa ushahidi mzuri juu ya marehemu Mwalimu Nyerere tena nitatoa kwa maandishi siyo kwa maneno pekee yake”alisisitiza. 
Ibada ya kumuombea Baba wa Taifa ilifanyika katika Kanisa la Mashahidi wa Uganda, Namugongo, ambapo ibada hiyo iliendeshwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Kampala, Dk. Cyprian Kizito Lwanga, ambaye aliiomba serikali kusaidia kuboresha eneo la kanisa hilo ili liwe na miundombinu ya kisasa zaidi. 
Hii ni mara ya nane ibada ya kuombea mchakato wa kumfanya baba wa Taifa kuwa Mwenyeheri na hatimye mtakatifu unafanyika katika kanisa hilo nchini Uganda. Mchakato huo ulianza mwaka 2006. 
 Katika ibada hiyo ambayo imehudhuria na maelfu ya Watanzania, pamoja na mataifa mbali mbali duniani, pia ilihudhuriwa na familia ya Marehemu Baba wa Taifa, Waziri Mkuu wa Uganda Amama Mbabazi mawaziri na wabunge kutoka Uganda, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Balozi wa Tanzania nchini Uganda.

No comments:

Post a Comment