.

.

.

.

Saturday, September 27, 2008

MARIAM WANGWE AOMBA MSAADA KWA SPIKA WA BUNGE

mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe, Mariam Zakayo Wangwe amemtaka Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, kuunda tume huru kuchunguza kifo cha mumewe kutokana na kutoridhishwa na uchunguzi wa polisi kuhusisha suala hilo na kosa la usalama barabarani.
Mbali na kumtaka Spika kufanya hivyo pia ameiomba serikali ifanye juu chini kuwasaidia katika uchunguzi wa kifo cha Wangwe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mariam alisema kuwa, hana imani na polisi kutokana na kuwa na rekodi mbaya katika masuala yao mbalimbali ya uchunguzi.
“Sipendi mambo haya yaishe hivi hivi na familia ya Wangwe hatujaridhishwa na namna polisi wanavyofuatilia kifo cha Wangwe kwa kuwa sina imani na polisi,” alisema Mariam.
Alisema kuwa kama polisi wanadai kuwa kifo cha Wangwe kimetokana na kosa la usalama barabarani basi hakuna haja ya Deus Mallya kuwekwa ndani.
Alisema ana wasiwasi na uchunguzi unaofanywa na polisi kwani hawajawahi hata kufika kumuuliza kuhusu kifo cha Wangwe akiwa kama mke wake.
“Hawajawahi kufika kutaka maelezo yangu labda ningewasaidia kwa kiasi fulani, katika maelezo ya Deus kuwa alikuwa amelala na Wangwe kukutwa kiti cha abiria basi atafutwe mtu wa tatu ambaye alikuwa akiendesha gari hilo,” alisema Mariam.
Alioneza, “Upelelezi ufanyike zaidi kwani hakijafanyika chochote hadi hivi sasa ajali ni ya ajabu na kama polisi wanasema ni kosa la usalama barabarani basi Deus Mallya aachiwe huru,”
Alidai kuwa aina ya kifo cha Wangwe kilivyotokea ni mambo yanayotokea Kenya hivyo huenda waliosababisha kifo hicho wametokea Kenya.
“Namna ajali ilivyotokea ni kama vile mambo yanavyotokea Kenya,” alisema.
Akizungumzia kuhusu hali ya mumewe mwezi mmoja kabla ya kifo chake Mariam alisema hali ilikuwa mbaya nyumbani kwake kutokana na Wangwe kuwa katika pilika pilika nyingi hasa baada ya kuenguliwa umakamu mwenyekiti wa Chadema.
Alisema, “Maisha ya Wangwe yalikuwa ya misukosuko sana dakika za mwisho”.
Kuhusu Chadema Mariam amekilaumu chama hicho kwa kutowajali tangu Wangwe afariki na kudai kuwa wanaweza wakawa wanahusika na kifo hicho kwani chuki yao kwa Wangwe wameipeleka mpaka kwa watoto.
Alisema chama hicho kimeitelekeza familia yao bila kujua kukubalika kwa chama hicho Tarime kunatokana na jitihada za Wangwe.
Alidai kuwa tangu Wangwe azikwe hakuna hata kiongozi mmoja wa Chadema aliyewahi kufika kuwajulia hali kitu ambacho kinahudhinisha.
Hata hivyo Mariam alisema kuwa kuamua kuzungumza na waandishi wa habari wakati huu hakuhusiani na kampeni za uchaguzi zinazoendelea jimboni Tarime.
“Tamko langu halihusiani na kampeni zinazoendelea Tarime kabisa kwani atakayechaguliwa hana msaada kwangu bali kwa wananchi wa Tarime,” alisema Mariam.

No comments:

Post a Comment