.
.
Sunday, September 21, 2008
MH. RAIS KIKWETE KUHUTUBIA UNTED NATIONS
RAIS Jakaya Kikwete ameondoka nchini Tanzania jana kwenda Marekani atakakohudhuria na kuhutubia kikao cha mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais kwa vyombo vya habari jana, Rais Kikwete amepangiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Septemba 23, kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Taarifa hiyo inaeleza zaidi kuwa akiwa Marekani, Rais Kikwete amepangiwa kuhudhuria mikutano mingine muhimu ukiwamo wa kuangalia mahitaji ya Maendeleo ya Malengo ya Milenia (MDGs). Atashiriki pia mijadala kuhusu afya ya mama na mtoto na ule wa ugonjwa wa malaria.
Septemba 26, Rais Kikwete atakwenda Washington atakakotoa hotuba muhimu ya ufunguzi wa kikao cha mwaka cha wabunge wenye asili ya Afrika, katika Bunge la Marekani. Atahutubia mkutano wa viongozi wa shughuli za biashara Marekani.
Mbali na mikutano hiyo, pia atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa, kibiashara na kiuchumi duniani.
Miongoni mwa viongozi atakaokutana nao kwa mazungumzo ni Rais wa Iran, Ahmedinajad, Katibu Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Javier Solana, na mfanyabiashara maarufu duniani, Bill Gates.
Pia atakutana na Waziri Mkuu wa Denmark, Anders Fogh Rasmussen, na Katibu Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Juan Somavia.
Shughuli nyingine atakazozifanya akiwa Marekani ni kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Sudan, Ustaz Ali Osman. Watazungumzia mgogoro wa eneo la Darfur.
Katika mazungumzo hayo, kwa pamoja wataangalia jinsi ya kuharakisha suala la kupeleka askari wa kulinda amani Darfur na jinsi ya kuahirisha angalau kwa mwaka mmoja, hati ya kukamatwa kwa Rais Omar A-Bashir wa Sudan, iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment