Hatima ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk. Edward Hoseah na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika, ambao wanachunguzwa na serikali kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Richmond, bado kitendawili kutokana na utetezi wao kuendelea kuchambuliwa. Mbali na Dk. Hoseah na Mwanyika, wengine wanaochunguzwa kutokana na kashfa hiyo, ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, maofisa wengine kadhaa wa serikali na wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Licha ya uchunguzi huo, vyombo vya dola pia vinawafuatilia waliokuwa mawaziri, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, ambao walijiuzulu Februari, mwaka huu kwa kuwajibika kisiasa, kuona kama walihusishwa na rushwa katika kashfa hiyo. Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alizungumza jijini Dar es Salaam jana kuwa utetezi wa viongozi na watendaji hao wa vyombo vya serikali, bado unaendelea kufanyiwa uchambuzi na kuwataka Watanzania waendelee kuvuta subira ili kuipa serikali nafasi ya kukamilisha uchambuzi huo. “Maelezo yao yanachambuliwa, uchambuzi bado unaendelea. Kama alivyosema Waziri Mkuu bungeni kuwa, wamepeleka maelezo kwa waajiri wao, sasa subiri waajiri wafanye kazi yao,” alisema Luhanjo. Hata hivyo, alipoulizwa lini uchambuzi huo unaweza kuwa umekamilika na taarifa kutolewa kwa umma, Luhanjo alikuwa mkali kuhusu swali hilo. ``Wewe unajua mwajiri wao (Dk. Hoseah na Mwanyika) ni nani?,`` aliuliza Luhanjo. Alipojibiwa kuwa ni Rais, Luhanjo alisema: ``Sasa unataka kumlazimisha Rais? Hujui kuwa huo ni utovu wa nidhamu?`` Luhanjo pia, alimlaumu mwandishi kwa kuhoji kuhusu hatima ya viongozi na watendaji hao wa vyombo vya serikali kwa kusema: ``Wewe kila siku tu unaulizia suala hilo, hauna jambo lingine?`` Alipojibiwa na mwandishi kuwa sababu ya kuulizia, inatokana na suala hilo kuwa ni la maslahi kwa umma, Luhanjo alisema: ``Hilo siyo public interest (maslahi ya umma), ni Personal Interest (maslahi ya mwandishi).`` Dk. Hoseah, Mwanyika na maofisa hao wa serikali na Tanesco, waliwasilisha utetezi wao kwa waajiri wao baada ya serikali kuwataka wafanye hivyo kutokana na kuhusishwa kwao na kashfa ya Richmond. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge juu ya mkataba baina ya Tanesco na Kampuni ya Richmond, bungeni, mjini Dodoma hivi karibuni. Kampuni hiyo ilishindwa kuwasilisha kwa wakati mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura wa megawati 100 na ilipofuatiliwa ikabainika ulikuwapo ukiukwaji katika kuipatia zabuni. Bunge liliunda kamati kuchunguza mchakato wa mkataba hio na ripoti yake ilipotolewa bungeni, ilisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri, Februari mwaka huu. Maazimio ya Bunge yalitokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe. Pinda aliwaambia wabunge kwamba Dk. Hosea alipelekewa barua ya kutakiwa kujieleza na Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu kwa nini yeye na wasaidizi wake wanane walishindwa kuona kuwa taarifa ya uchunguzi iliyofanywa na wataalamu wa taasisi yake haikuona kasoro zilizokuwa kwenye zabuni ya Richmond. Kwa mujibu wa Pinda, watumishi hao wa Takukuru walitakiwa kutoa maelezo ya kwa nini waliona kwamba uteuzi wa Richmond ulizingatia sheria, kanuni na taratibu za serikali; hakukuwa na upungufu katika zabuni na taifa halikupata hasara kutokana na zabuni hiyo. ``Wote tisa wamewasilisha utetezi wao katika muda uliopangwa. Aidha kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu wa Utumishi wa Umma, mamlaka yao ya nidhamu inapitia utetezi wao kutoa uamuzi unaostahili,`` alisema Pinda. Alisema Dk. Hosea na wengine walioandikiwa barua za kutakiwa wajieleze wamefanyiwa hivyo kwa kuzingatia misingi ya kanuni asilia ya haki ya kusikilizwa kwanza kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa. Kuhusu azimio lililomtaka Mwanyika awajibishwe na Rais kutokana na mkataba wa Tanesco na Richmond kusheheni makosa mengi ya kisheria yanayoonyesha udhaifu wa kitaalamu kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Waziri Mkuu alisema: ``Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye alikuwa miongoni mwa watendaji wakuu watatu waliokuwa wanaishauri Serikali, suala la kuhusishwa kwake na mchakato mzima wa mkataba huo linashughulikiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu.`` Wengine ambao Waziri Mkuu Pinda alisema maelezo yao kuhusu ushiriki wao katika mchakato wa Richmond yamepokewa na yanafuatiliwa, ni wajumbe wa kamati tatu za majadiliano ya mkataba. Aliwataja hao kuwa ni Mwanyika, Mgonja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, ambao kamati yao ilikuwa na jukumu la kutoa ushauri kwa Waziri wa Nishati na Madini na serikali kwa jumla.
No comments:
Post a Comment