Serikali inatarajia kuingia ubia na Shirika la Ndege la China Sonangol (CSIL) kwa ajili ya kuliendesha Shirika la Ndege Tanzania (ATC). Hadi sasa mazungumzo kati ya serikali na shirika hilo yanaendelea na yamefikia kiwango cha juu cha kuridhisha. Kuungana huko kutakuwa kwa mara ya pili kwa ATC iliyoungana na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na kuitwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), iliyovunjika miaka miwili iliyopita. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mohamed Missanga aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa shirika hilo linalazimika kuingia ubia kutokana na sasa kuwa katika hali mbaya kiuendeshaji. Alisema wakati ndoa kati ya SAA na ATC inavunjika, serikali iliahidi kuchukua madeni ya ATC na kuipatia mtaji ili ijiendeshe vizuri, ahadi ambayo haijaitekelezwa hadi leo. “Kutokana na yote hayo kutofanyika, hivi sasa ATC haifanyi vizuri, haikopesheki kwa sababu vitabu vyake vya hesabu vinaonyesha ina madeni. Sasa ATC inalazimika hata kununua mafuta kwa fedha taslimu wakati mwingine inakuwa haina fedha kwa wakati husika,” alisema. Hata hivyo, Missanga ambaye ni Mbunge wa Singida Kusini (CCM), alisema serikali imeshaanza kuhangaika kutafuta kulipa deni hilo na kutolea mfano, imechukua hatua ya kuiandikia barua SAA kutowasumbua ATC juu ya deni hilo na badala yake waidai serikali. Missanga alikuwa akizungumza baada ya kumaliza mkutano na viongozi wa ATC akiwamo Mwenyekiti wa Bodi, Mustapha Nyang’anyi na Mkurugenzi wake, David Mattaka, pamoja na viongozi wengine wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu. Kamati hiyo iliishauri serikali kuwa makini na mwekezaji huyo kwa kuhakikisha mkataba inayoingia nayo hauna kasoro, unaozingatia maslahi ya Watanzania ili makosa yaliyotokea kwa SAA yasijirudie na kuitaka kuharakisha mazungumzo hayo. Kuhusu wabunge kuuona mkataba huo, Missanga alisema, “serikali imeshatuambia tunaweza kuiona mikataba mbalimbali ila kwa utaratibu wa Spika kuiomba serikalini.” Wakati inajiandaa kuingia ubia, ATC imeanza mchakato wa kuuza ndege yake aina ya Boeing 737-200 ambayo inadaiwa inatumia mafuta mengi. Ndege hiyo ilirithiwa kutoka Shirika la Ndege la Afrika Mashariki. Mbali na ndege hiyo, shirika hilo lina ndege tatu zinazofanya kazi ambapo mbili ni zake na moja imekodi.
No comments:
Post a Comment