Mwili wa binti uliokutwa kwenye kiroba watambuliwa
Hatimaye ule mwili wa mrembo aliyeuawa kikatili kwa kukatwa vipande, kuwekwa katika kiroba na kisha kutupwa bondeni pale Tabata Chang`ombe umetambuliwa rasmi na ndugu na jamaa za marehemu. Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Pius Sheka amesema mwili huo umetambuliwa kuwa ni wa Rehema Mushi, mkazi wa Tabata Chang`ombe. Kamanda Sheka amesema walioutambua mwili huo ni ndugu wa marehemu ambao walifika katika eneo la tukio na kuuona mwili huo kabla ya Polisi kuuchukua. Akasema ingawa mwili wa marehemu ulikuwa umeharibika vibaya, wao waliupeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako madaktari waliufanyia uchunguzi. Akasema hivi sasa Polisi wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa daktari ili kubaini chanzo cha kifo cha mtu huyo. Hata hivyo, akasema makachero wake pia wanaendelea na upelelezi wa kipolisi ili kubaini chanzo cha kuuawa kikatili kwa mrembo huyo. Awali, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubombolwa, Bw. Heri Mdundo amesema mwili wa marehemu huyo ulitambuliwa na mama yake mzazi. Hata hivyo, akasema mama huyo aliyedai kuwa mwili wa marehemu ni wa mwanawe, si mkazi wa Mtaa wao wa Ubombolwa. ``Huyo mama aliyeutambua mwili wa marehemu sio mkazi wa eneo langu. Amesema anatokea maeneo ya Kisukuru... sikuweza kupata jina lake kwa sababu alikuwa akilia sana kutokana na uchungu wa kifo hiki,`` akasema Bw. Mdundo.
SOURCE: Alasiri
No comments:
Post a Comment