Kampuni ya DMB inatarajia kuanzisha shindano liitwalo Maisha Plus litakaloanza Desemba mwaka huu na kushirikisha washiriki 18 kutoka mikoa tisa nchini. Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa Wakurugenzi wa bodi wa kampuni hiyo Masoud Kipanya alisema kuwa shindano hilo la aina yake linafanana na lile la Big Brother Africa linaloendeshwa Afrika Kusini. Kipanya alivitaja vigezo vitakavyotumika kuwapata washiriki hao kuwa ni wale wenye umri kati ya miaka 18 hadi 27 na pia watazingatia mwonekano, ujasiri, ukakamavu na masuala mengine muhimu. Alisema wameanza matayarisho ya ujenzi wa kijiji kitakachotumiwa na washiriki hao, eneo la Geza Ulole, Kigamboni. Kipanya alisema katika shindano hilo mshindi ambaye atapatikana kwa kura za wananchi atazawadiwa Sh milioni 10. Akizungumzia undani wa shindano hilo alisema washiriki hao watakaa ndani ya jumba hilo kwa mwezi mmoja kabla ya watu kupiga kura za kumtoa mshiriki mmoja baada ya mwingine. Kipanya aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Morogoro, Dodoma, Mwanza, Arusha, Tanga, Mbeya, Mtwara, Iringa na Zanzibar na fomu za ushiriki zitaanza kutolewa wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment