KITUO cha Televisheni ya kulipia, GTV hakitaonyesha laivu pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga Jumapili katika Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na sababu za ratiba ambazo pia zipo nje ya uwezo wao na badala yake watarekodi na kuuonyesha baadaye.
Mchezo huo ambao awali ulikuwa urushwe laivu na kituo hicho imeshindikana na tayari wamelitaarifu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa hawataweza kufanya hivyo kutokana na ratiba zao kuingiliana na kwamba wataurekodi na kuuonyesha baadaye.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu TFF, Fredrick Mwakalebela alisema kwa niaba ya wapenzi wa mpira wa miguu wanaishukuru serikali kwa kutoa kibali cha kuruhusu mchezo huo kufanyika katika uwanja mpya.
Mwakalebela hata hivyo, alivitaja viingilio katika mchezo huo kuwa ni Sh20,000 kwa wakubwa (VIP A), Sh15,000 VIP B, Sh 10,000 kwa VIP C.
Kwa upande wa viti vya rangi ya machungwa nyuma ya magoli, Mwakalebela alisema itakuwa Sh5000 na mizunguko yote miwili ya viti vya rangi ya bluu na kijani ambako hukaa watazamaji wa kipato cha chini itakuwa Sh3000.
Alisema viingilio hivyo vimepangwa kuwa chini kwa nia ya kuwapa fursa mashabiki wengi kujitokeza kwa wingi kuona pambano hilo ambalo lina mvuto wa aina yake na wa kipekee.
Aidha, alisema tiketi zitaanza kuuzwa kesho katika vituo mbalimbali ambavyo vitatangazwa baadaye na shirikisho hilo.
Katibu huyo wa TFF alisema kabla ya pambano hilo la Simba na Yanga kutakuwa na mechi ya ufunguzi kati ya maalbino na wabunge.
No comments:
Post a Comment