Mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari Kanoge wilayani Mpanda, mkoani Rukwa amekufa baada ya kuchomwa kisu mgongoni na mwanaume mmoja aliyekataa kufanya naye mapenzi. Taarifa zilizotolewa na kuthibitishwa na jeshi la polisi wilayani Mpanda, zimemtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Grace Mgawanyu (23), ambaye alichomwa kisu na Bakisi Buruga (28) ambaye naye alijiua muda mfupi baada ya kutenda unyama huo. Taarifa zimeeleza kuwa siku ya tukio Oktoba 29, Grace alikuwa akitokea shule akiwa amepakizwa kwenye baiskeli na rafiki yake wa kike wakiwa wanaelekea nyumbani, wakiwa njiani, walikutana na mwanaume huyo waliyempita kwa kasi lakini alirusha kisu na kumchoma mwanafunzi huyo mgongoni kisha kudondoka chini huku akitokwa na damu nyingi. Baada ya kudondoka chini mwanaume huyo alimfuata mwanafunzi huyo na kumshambulia tena kwa kumchoma kisu katika mikono huku akimweleza kuwa mwisho wa maringo yake ulikuwa umefika, na atajutia kumkataa kushirikiana naye kimapenzi. Shambulio hilo lilimfanya mwanafunzi aliyembeba Grace katika baiskeli kuanza kupiga kelele zilizowakusanya wanafunzi wengine waliokuwa katika masafara wa kurudi makwao, hatimaye walianza kumfukuza Buruga aliyekuwa akitokomea porini. Akiwa amekimbia umbali mrefu ili hali wanafunzi hao wakizidi kumkimbiza Buruga alisimama huku akitweta na kusema kuwa ni bora afe kuliko kutiwa mikononi mwa wanafunzi hao au polisi, ndipo alipochomoa kisu chake na kujichoma mwenyewe tumboni kwa kujichana katikati ya tumbo akitenganisha sehemu ya tumbo na mbavu na hatimaye alidondoka chini na kufa papo hapo. Wakiwa wanashuhudia kwa karibu muuaji huyo akijiua mwenyewe, wanafunzi hao wa shule ya Sekondari Kanoge waliondoka hadi sehemu alipochomwa kisu mwenzao na kumkuta akigalagala chini kwa maumivu ambapo walitoa taarifa kituo cha polisi waliokwenda kumchukua na kumkimbiza hospitali ya wilaya ya Mpanda wakiwa na maiti ya Buruga. Habari zilieleza kuwa mwanafunzi huyo alifariki dunia akiwa njiani akikimbizwa hospitalini kupata matibabu. Uchunguzi wa polisi wilayani Mpanda ulibaini kuwa awali baada ya kumkataa mwanaume huyo Grace alitumiwa ujumbe kupitia kwa rafiki wa Buruga ukimwarifu kuwa akae chonjo kwani hakukubaliana na maamuzi ya kukataliwa licha kubembelezwa kwa muda mrefu hivyo aliahidi kumfanyia kitu kibaya katika maisha yake. Hata hivyo, polisi walisema walishangazwa na mwanafunzi huyo kutotoa taarifa katika vyombo vya usalama licha ya kupokea vitisho hivyo kutoka kwa mwanaume huyo
No comments:
Post a Comment