.

.

.

.

Sunday, January 11, 2009

AJALI YAUA 27 PAPOHAPO WILAYANI KOROGWE


Watu 27 wamekufa papo hapo na wengine 23 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi la abiria Kampuni ya Tashrif walilokuwa wakisafiria, kuligonga lori la magogo katika Kijiji cha Hale-Kijijini wilayani Korogwe, mkoani Tanga. Hiyo ni ajali kubwa ya pili tangu kuanza kwa mwaka huu, baada ya Januari 4, mwaka huu, kushuhudia watu 11 wa familia moja wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kufariki kwa ajali ya gari eneo la Uchira Moshi Vijijini, wakitokea katika shughuli ya kipaimara wilayani Hai. Ajali ya Tashrif ilitokea juzi saa 2:30 usiku katika Barabara Kuu ya Muheza -Segera wakati basi hilo lilipokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Tanga. Kati ya majeruhi hao, wawili hali zao ni mbaya sana na wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza. Basi hilo la Tashrif lenye namba ya usajili T768 ALW lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja tu la Mdoe au maarufu Osama, liliacha njia na kulivamia lori la magogo aina ya Isuzu Scania lenye namba za usajili T594 APA lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara hiyo. Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Simon Sirro alisema dereva wa basi hilo alikimbia baada ya tukio hilo na wafanyakazi wengine watatu wa basi hilo waliokuwamo kwenye gari wakati wa tukio, wamefariki dunia papo hapo. Kamanda Sirro alisema chanzo cha ajali hiyo, ya pili kubwa mkoani Tanga ikitanguliwa na ile ya basi la No Challenge la mwaka 1998, lililoua abiria wapatao 70, ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi hilo na uchunguzi unaendelea. No Challenge lilibadilishwa jina na kuitwa Tashrif.

No comments:

Post a Comment