Rais Jakaya Kikwete jana alikwepa kumtunuku mmoja wa watuhumiwa wa kesi za wizi wa fedha katika akaunti ya madeni ya nje(EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania(BoT), wakati akitakiwa kugawa pikipiki kwa makatibu wa Chama cha Mapinduzi wilayani hapa. Rais alikwepa kugawa pikipiki hizo zenye thamani ya sh.milioni 24.5 baada ya kubaini uchangiaji huo ulijumuisha mfadhili ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa mafuta, Japhet Lema maarufu kama Njake, anayetuhumiwa katika wizi wa fedha EPA. Mfanyabiashara huyo alihudhuria hafla hiyo ili naye atunukiwe cheti cha shukrani. Pikipiki hizo ambazo zimekaa kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa katika ofisi ya CCM wilayani Arusha zikitafuta \'mzito\' wa kuja kuzigawa, zilikuwa zikabidhiwe sanjari na vyeti vya shukrani kwa waliozitoa,katika shughuli iliyoandaliwa na chama hicho wilaya. Kwa mujibu wa habari za ndani ya chama hicho, waliochangia pikipiki hizo kumi na tisa ni pamoja na mbunge wa Arusha Felix Mrema na mwenyekiti wa CCM wilayani Arusha Jubilate Kileo. Rais Kikwete pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, aliwasili katika uwanja wa CCM wilayani hapa majira ya saa kumi jioni na baada ya kukaribishwa kuzungumza, ikitegemewa baadaye ndipo ataanza kazi ya kugawa pikipiki hizo, akasema kamwe hataweza kufanya hivyo bali atawaachia viongozi wa wilaya wajigawie wenyewe. ``Nimeziona lakini sitaweza kugawa moja baada ya nyingine, mimi sijui mlikozipata, lakini wenyewe mnajua mtakaa mtagawana wenyewe,``alisema.
No comments:
Post a Comment