MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeongeza gharama ya kuhifadhi makontena bandarini kwa asilimia 100 kuanzia jana. Vilevile TPA imetangaza kwamba itapiga mnada makontena yaliyokaa kwa muda mrefu bandarini bila ya kuchukuliwa na wahusika. Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa Bandari, Peter Milanzi alitoa taarifa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana. Milanzi alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya wateja kutochukua makontena kwa wakati na kusababisha msongamano wa meli nje ya mlango wa bandari. "Kuanzia leo Januari mosi (jana) gharama ya kuhifadhi makontena bandarini imeongezeka na kwamba kontena litakalokaa bandarini baada ya siku 21, gharama yake itakuwa dola za Marekani 40 (zaidi ya Sh 51,000) kwa kontena la futi 20 na dola 80 kwa kontena la futi 40,” alisema Milanzi. Aidha, alisema makontena yote yaliyokaa kwa muda mrefu bandarini zaidi ya siku 21 kama hayatachukuliwa ifikapo Januari 15 mwaka huu, yatakabidhiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kupigwa mnada. Milanzi alisema upigaji mnada makontena hayo utafanyika kwa haraka na hatua hiyo itakuwa endelevu. Aliwataka wateja kwenda kuyaondoa makontena hayo haraka kabla ya kazi hiyo kuanza. Alisema TPA pamoja na wadau wake wataendelea kufanya kazi kwa saa 24 kila siku ili kuwezesha wateja wao kuchukua mizigo muda wote wanapotaka kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment