Hali ya wasiwasi inazidi kuongezeka Mashariki ya Kati baada ya roketi kuvurumishwa kutokea Lebanon na kuangukia Israel, hali inayotishia kuenea kwa mzozo huo.
Jeshi la Israel lilijibu shambulio hilo kwa kufyatua mizinga kuelekea sehemu tatu zilizorushwa roketi hizo. Hadi sasa hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na shambulio hilo.
Vyombo vya habari vya Israeli baadae viliarifu kutokea shambulio la pili la roketi, lakini msemaji wa jeshi alisema kulikuwa na makosa ya kingora cha kuashiria hatari.
Mashambulio hayo yamekuja huku ndege za jeshi la Israel zikiwa zimefanya mashambulio 60 katika Ukanda wa Gaza usiku kucha, zikilenga maeneo yanayotumiwa na wapiganaji wa Hamas.
Wachambuzi wa mambo wanaona hiki ni kipindi cha hatari katika mzozo huo unaoendelea.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC eneo la Mashariki ya Kati, Jeremy Bowen shambulio la roketi kutokea Lebanon yanaweza kuchochea kupanuka zaidi kwa vita.
Haijaeleweka vyema iwapo roketi hizo zilivurumishwa na kundi la Hezbollah au moja ya makundi ya wapiganaji wa Kipalestina yenye makao Lebanon.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC iwapo Hezbollah watakuwa wamefanya shambulio hilo, basi kuna hatari huenda Israel ikajibu kwa hasira kubwa.
Wapalestina waliopo Lebanon hawana uwezo wa kupigana vita na Israel lakini Hezbollah wanao uwezo huo.
Wakati huohuo juhudi za kidiplomasia kumaliza mapigano ya Gaza zimeendelea ambapo afisa mwandamizi wa serikali ya Israel anaelekea Cairo Misri kusikiliza yaliyomo katika mpango wa amani ulioandaliwa kwa pamoja na Misri na Ufaransa.
No comments:
Post a Comment