.

.

.

.

Monday, February 23, 2009

KOMAL KATAKIA AJINYONGA GEREZANI ???

UTATA umetawala kuhusu maisha ya mke wa mfanyabiashara Vinoth Praven (23) raia wa India aitwae Komal Katakia (22)Pichani juu, ambaye anashikiliwa na Jeshi la Magereza katika gereza moja jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara Abdulbasiti Abdallah (21), huku taarifa za awali zikieleza amefariki dunia na zingine zikisema kuwa yu hai gerezani.

Habari za kifo cha Komal zilianza kuenea jijini hapa kuanzia juzi Ijumaa huku baadhi ya watu wakidai kuwa ameuawa na wengine wakidai kuwa amejinyonga, lakini msemaji wa Jeshi la Magereza, Omari Mtiga alikanusha taarifa hizo akidai kuwa amewasiliana na maafisa wa magereza ambao wamemuhakikishia kuwa hawana taarifa hizo.

Habari kutoka kwa jamaa wa karibu wa Komal zinadai kuwa amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kitambaa cha kichwa (mtandio).
"Komal amekufa tangu juzi (Ijumaa) lakini tunashangaa mpaka sasa serikali haijataka kutoa taarifa za kifo chake na hata magazeti hayajaandika" alisema mmoja wa jamaa hao na kuongeza.
"Mimi nilidhania kuwa magazeti ya leo (jana) yangeandika taarifa za kifo hiki, lakini nimeangalia hakuna gazeti hata moja lililoandika, sijui tatizo nini".
Alipoulizwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hawezi kuzungumzia kifo hicho kwani mtuhumiwa huyo hakuwa mikononi mwao.
"Siwezi kuzungumzia habari za kifo cha mtuhumiwa huyo, waulizeni magereza kwani hizi ni mamlaka mbili tofauti" alisema Kamanda Kova na kuongeza:
"Ok, sisi tukisema amekufa halafu magereza wakikanusha kuwa hajafa? Lakini pia mpaka sasa hatujaletewa barua kuwa amekufa au la, kwa hiyo hatuna ushahidi".

Juhudi za kuwapata maofisa wa magereza kuthibitisha kifo hicho hazikufanikiwa baada ya ofisa mmoja kupigiwa simu, ambapo mara baada ya kuulizwa swali alikata simu hiyo na kukataa kupokea tena kila alipopigiwa na mwandishi.
Hata hivyo baadhi ya vyanzo vya habari hii vimedokeza kuwa mtuhumiwa huyo amekufa na maiti yake imepelekwa Hospitali ya Rufaa Muhimbili ikiwa na makovu.
"Inadaiwa kuwa amekufa kwa mateso, kwa sababu mwili wake umeharibika kwa mateso na una makovu mengi," kilidokeza chanzo cha habari.

Febuari 8 mwaka huu Polisi jijini Dar es Salaam walimtia mbaroni raia wa India, Vinoth Praven (23) na watu wengine wanne akiwamo mke wa raia huyo, Komal Katakia (22), kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara Abdulbasiti Abdallah (21), ambaye mwili wake ulikutwa ndani ya begi la nguo katika Jengo la Harbour View, Mtaa wa Samora.

No comments:

Post a Comment