.

.

.

.

Friday, February 27, 2009

MH.NGELEJA ADAI SI UFISADI !!!

Waziri William Ngeleja amesema kuwa kununua mitambo michakavu ya DOWANS hakutakuwa na chembechembe zozote za ufisadi ingawa wengi wanahisi hivyo.
"Nchi haiongozwi kwa hisia," alisema Ngeleja, ambaye alitetea sana mpango wa kununua mitambo hiyo wakati akiongea na waandishi kuhusu uamuzi wa serikali kukubaliana na ushauri wa kamati ya bunge wa kuzuia kununuliwa kwa mitambo hiyo.
"Ni hatari kuacha kujadili mambo muhimu ya nchi yanayozingatia maslahi ya taifa, na badala yake kuendekeza hisia zisizo na mantiki,"alisema.
Ngeleja alisema kitendo cha watu kuhisi kuna kuna ufisadi katika mpango huo wa kununua mitambo hiyo, hakina mantiki, akisema kuwa serikali iko makini na haiwezi kukubali matokeo kama ya Richmond, ambayo ilipewa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa mazingira tata na kusababisha Bunge kuingilia kati na kufanya uchunguzi uliosababisha Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu na baadaye kufuatiwa na mawaziri wawili.
Ngeleja alisema vipo vyombo vya serikali vinavyosimamia sheria na vinafanya kazi kwa umakini na akahoji: "Hivi watu hawaoni vigogo wanavyoburuzwa mahakamani, sasa watu wanafikiri serikali imelala, kwanini tuendeshe nchi kwa hisia."
Alipoulizwa kama kuna msukumo wowote kutoka kwa watu ambao walituhumiwa kuhusika katika mpango wa kuifanikisha Richmond kushinda zabuni ya ufuaji umeme wa dharura, Ngeleja alijibu: "Umeangalia maslahi ya taifa tu."
Ngeleja alisema msukumo wa kutaka kununua sasa mitambo hiyo unatokana na kuangalia ukuaji wa uchumi, ambao mahitaji yake ya umeme yanaongekeza kwa asilimia kati ya 10 hadi 15 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008 hadi 2012.
"Utafiti uliofanywa katika Power System Master Plan (mpango wa kuendeleza sekta ya umeme) unaonyesha mahitaji ya umeme yanakua kwa wastani wa asilimia 10 hadi 15 kila mwaka katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008 hadi 2012," alisema.
Alisema changamoto ni kwamba mipango iliyopo ya kuongeza uzalishaji haitaweza kuziba pengo kati ya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme na mahitaji ya umeme yanayotarajiwa kati ya mwaka huu na mwaka kesho, baada ya miradi ya dharura kuondolewa.
"Hii inatokana na ukweli kwamba, ni vigumu kubuni mradi unaoweza kukamilika kabla ya mwaka 2009 kuisha," alisisitiza.
Kuhusu bunge kushauri mitambo hiyo ya Dowans isinunuliwe kutokana na kwenda kinyume na sheria ya manunuzi ya umma, Ngeleja alijibu: "Ninachokumbuka, bunge lilijadili na kupitisha azimio kuhusu uhalali wa mkataba wa Richmond.
"Hakuna mtu anayepinga... mkataba wa Richmond ulibainika kuwa tata na serikali ilichukua hatua. Serikali haiwezi kuzembea wala kufumbia macho vitendo vya kifisadi.
"Juni 28, 2008 serikali ilitoa tamko la kusitishwa mkataba huo ifikapo Agosti mosi na kweli ilifanyika... hatua hiyo ilichukuliwa na serikali lakini pia kwa kuzingatia maelekezo ya bunge," alifafanua.
Alipoulizwa sababu za kung'ang'ania kununua mitambo hiyo kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umme ambayo inazuia taasisi za serikali kununua mitumba, Ngeleja alihoji: "Mbona watu wanasema tununue mitambo ya IPTL.
"Ni kweli sheria ya PPRA inatakaza ununuzi wa vitu vilivyotumika, lakini yapo maeneo ambayo kutokana na mazingira halisi ya kisekta si lazima kinachonunuliwa kiwe kipya.
"Angalia, ATC leo hii inaweza kununua au kukodi ndege lakini si lazima iwe mpya. Tuangalie maeneo ya msingi, jambo kubwa ni watalaamu kuthibitisha ubora na uwezo wa kukidhi mahitaji ya nchi. Mitambo ile unaweza kuifunga leo hii katika toroli na kuipeleka mkoa wowote wenye uhaba wa umeme."

No comments:

Post a Comment