.

.

.

.

Thursday, February 26, 2009

MKE AUWA MUME AKISHIRIKIANA NA HAWARA

WATU watatu wakazi wa kitongoji cha madukani kijiji cha Nyiberekera kata ya Isenye wilayani Serengeti wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua kikatili mtu mmoja mwenye umri wa miaka 64 baada ya kumchinja na baadaye kutumbukiza mwili wake chooni.
Kati ya watu hao, ambao majina yao tumeyahifadhi, yumo mke wa marehemu anayedaiwa kushirikiana na hawara yake kumuua kikatili mumewe Moshi Nyibu.

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Nyiberekera, Tariani Gesura amesema kuwa mwili wa marehemu uligunduliwa juzi majira ya saa 4:00 asubuhi kwenye choo na mtu aliyemtaja kwa jina la Nyaruhembe Sabure(15) ambaye huchunga mifugo ya Nyibu. Mchungaji huyo wa mifugo alikuwa akienda chooni kujisaidia ndipo alipokuta mwili wa Nyibu ukiwa na jeraha kubwa shingoni kutokana na koromeo lote kukatwa na ndipo alipotoa taarifa kwa familia yake.

Ofisa huyo alisema kuwa anahisi waliofanya tukio hilo walikuwa na nia ya kuutumbukiza chooni mwili huo wa Nyibu, lakini wakashindwa na kuutelekeza.
Alibainisha kuwa taarifa hiyo ilimfikia mtoto wa marehemu aliyemtaja kwa jina la Jumamosi Nyibu aliyekuwa dukani kwake na alipofika chooni alikuwa watu wengi wameshakusanyika.
“Eneo la tukio ni hapo nyumbani. Mkewe huyo alikuwepo tena aliwahi mapema sana kufua, kitu ambacho ni tofauti na siku nyingine," alisema ofisa huyo. "Pia aliwahi sana kudeki ndani na ndio maana watu walihisi kitu na hivyo kufuatilia na kugundua michirizi ya damu ikitokea ndani ya nyumba ya marehemu,” alisema.

Mtendaji huyo alisema polisi wa kituo kidogo cha Issenye walifika eneo la tukio na kuwachukua watuhumiwa hao kwa ajili ya mahojiano zaidi kutokana na mazingira ya utata juu ya kifo cha mzee huyo.
Baadhi ya majirani wa Nyibu walidai kuwa kijana huyo, mkazi wa Bunda eneo la Nyansura, amekuwa na mahusiano ya kipenzi na mwanamke huyo kiasi kwamba kumekuwa na kutokuelewana ndani ya ndoa.
Walidai kuwa muuaji asingeweza kutoka nje ya eneo hilo kutokana na hali ya ulinzi ilivyo nyumbani kwa marehemu, ambayo ina mbwa wakali ambao hufanya majirani kutozoea kuingia ndani ya uzio huo.


Majirani hao walidai kuwa uhusiano wa kijana huyo na mwanamke huyo ulianza muda mrefu kiasi kwamba ilifikia hatua ya mwanamke huyo kulala vyumba tofauti na mumewe.
“Mke huyo amekuwa akisemwa lakini hajirekebishi labda ni kutokana na umri wake na huyo marehemu ambaye alizaa naye mtoto mmoja... pamoja na kuwa na watoto wawili ambao si mzee huyo, alikubali kuwatunza,” alisema shuhuda mmoja.

Watuhumiwa hao wanategewa kufikishwa mahakamani ili kusomewa mashitaka kuhusiana na tuhuma hizo na mwili wa Nyibu unatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwake.

No comments:

Post a Comment