.

.

.

.

Sunday, February 01, 2009

NAULI MPYA RELI YA KATI

Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imetangaza kupandisha nauli za treni za abiria kwa asilimia 11.6 kwa madaraja yote kuanzia Februari 15 mwaka huu. Nauli hizo zilizoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) zitatozwa kulingana na umbali wa kituo hadi kituo kati ya Dar es Salaam na Kigoma na ya chini itakuwa Sh 6,200 na ya juu itakuwa Sh 60,600. Taarifa ya uongozi wa TRL kwa umma imeeleza kuwa kiwango hicho kipya cha nauli hakitahusisha huduma mpya ya daraja la tatu zinazotarajiwa kuanza Februari saba mwaka huu.
Kwa mujibu wa tangazo la kampuni hiyo iliyo chini ya uongozi wa Kampuni ya Rites ya India, abiria wa daraja la tatu watalipa kati ya Sh 6,200 na Sh 19,200, daraja la tatu kulala watalipa kati ya Sh 7,700 na Sh 24,000.
Daraja la pili kulala watalipa kati ya Sh 13,300 na Sh 44,400
Daraja la kwanza kulala watalipa kati ya Sh 16,900 na Sh 60,600.
Awali abiria waliosafiri kwa mabehewa ya daraja la tatu walilipa kati ya Sh 3,300 na 17,100, daraja la pili kati ya Sh 3,400 na Sh 39,700 na daraja la kwanza walilipa kati ya Sh 7,600 na Sh 54,300 kwa kuzingatia umbali wa kituo anachoanzia safari hadi anapoteremkia. Nauli mpya zilizotajwa katika taarifa hiyo, zinahusu Kituo Kikuu cha Dar es Salaam kwenda Morogoro, Dodoma, Tabora, Isaka, Shinyanga, Mwanza, Urambo, Kaliua, Nguruka, Uvinza na Kigoma. “Nauli mpya ya daraja la tatu kulala ni za kuanza tu. Haya mabehewa yaliyoingizwa nchini hivi karibuni yatatumika kwa huduma za abiria za treni za moja kwa moja ‘Express’ tu hakuna ongezeko la nauli katika huduma hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Kwa mujibu wa TRL, treni hizo za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza zitakuwa za aina mbili kwa kutumia mabehewa ya daraja la tatu kulala. Kampuni hiyo ilisema, treni hizo zitapunguza muda wa safari kwenda na kurudi kwa saa nne na zitaondoka Dar es Salaam kila Jumanne na Ijumaa kwenda Kigoma na Mwanza na kila Jumapili kwenda Kigoma.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa, treni za Express zitakuwa zikiondoka Dar es Salaam kila Jumatano kwenda Kigoma tu, na kila Jumamosi itatoka Dar es Salaam kwenda Mwanza tu, saa 11 jioni. TRL ilieleza kuwa treni za abiria za moja kwa moja zitasimama katika vituo vya Morogoro, Kilosa, Dodoma, Saranda, Manyoni, Tabora, Urambo, Kaliua, Nguruka, Uvinza, Kigoma, Isaka, Shinyanga na Mwanza. “Abiria ataruhusiwa kuchukua mzigo wake binafsi usiozidi kilo 30 katika huduma za treni za abiria za moja kwa moja ‘Express Train Service’, ambazo mabehewa ya daraja la tatu kulala yatatumika,” ilisema taarifa hiyo na kubainisha kwamba, kuanzia Machi mosi mwaka huu, huduma ya treni ya abiria ya Jumapili kwenda Kigoma itatumia mabehewa ya daraja la tatu kukaa. TRL ilianza kutoa huduma za reli Oktoba mosi mwaka juzi baada ya kusaini makubaliano na serikali Septemba tatu mwaka huo, kuiruhusu Kampuni ya Rites kutoka India kuchukua majukumu ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

No comments:

Post a Comment