Watu wawili akiwamo dereva wa pikipiki ya magurudumu matatu aina ya Bajaj ambaye hajafahamika na abiria Juma Ulaya (21), wamekufa na wengine watano kujeruhiwa baada ya kugongwa na gari juzi jijini Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 1 usiku eneo la Kariakoo. Ajali hiyo ilitokea wakati gari namba T740 AQQ aina ya Toyota Sprinter lililokuwa likiendeshwa na Harsheel Shaa (24), lilipogonga Bajaj hiyo yenye namba T288 ABH. Kamanda Shilogile alisema kuwa abiria na dereva huyo walikufa papo hapo wakati abiria wawili kati ya watano ambao ni Dubisi Robert (60) na Juma Iddy (63), wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Aidha abiria watatu ambao hawakufahamika majina yao walitibiwa hospitali hapo na kuruhusiwa na mwili wa dereva wa Bajaj umehifadhiwa Hospitali ya Amana wakati wa Ulaya umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na dereva Shaa amekamatwa na polisi.
Wakati huo huo, Mwendesha mkokoteni asiyefahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (30-35) amekufa baada ya kugongwa na gari lisilofahamika. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Kandihabi, alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 2 usiku eneo la Magengeni ambapo gari lisilofahamika lilimgonga mwendesha mkokoteni huyo na kufa papo hapo. Mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Temeke.
No comments:
Post a Comment