.

.

.

.

Friday, August 14, 2009

MAOFISA DECI WAACHIWA HURU

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imewaachia huru kwa dhamana wachungaji wengine wawili wa DECI baada ya kukamilisha masharti.
Wachungaji hao, walioachiwa huru jana na Hakimu Mkazi, Nyigulile Mwaseba mara baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ni Samuel Sifael na Arbogast Kipilimba.
Kabla ya washtakiwa hao kuachiwa huru Wakili Mwandamizi wa Serikali, Justus Mlokozi alidai kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kuomba ipangiwe tarehe nyingine.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwaseba aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 9, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Uamuzi huo unatolewa baada ya Agosti 12, mwaka huu hakimu mkazi, Waliarwande Lema kuwaachia huru viongozi watatu wa Deci mara baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Justus Mlokozi kudai kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na hati ya kuomba kuongezewa muda kutoka kwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na hati ya kuondoa pingamizi la dhamana kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 148 (4) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Waliochiwa kwa dhamana juzi ni Jackson Sifael, Dominick Kigendi, Timoth Sangura ambao wote walikamilisha masharti ya dhamana.
Viongozi hao ambao pia ni wachungaji wa madhehebu ya Kanisa la Pentekoste wanaokabiliwa na mashtaka ya kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume cha sheria (DECI).
Akiwaachia kwa dhamana hiyo juzi, Hakimu Lema alisema kutokana na hati iliyowasilishwa mahakamani hapo kutoka kwa DPP chini ya kifungu cha 148(4)cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai inaonyesha kuwa hana pingamizi tena la dhamana dhidi ya washtakiwa hao.
Hivyo aliwataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini wawili wanaominika kwa kila mmoja wao na kwamba, mmoja kati ya wadhamini hao awe mkazi wa jijini Dar es Salaam na kila mdhamini asaini bondi ya Sh 10 milioni.
Pia aliwataka wawasilishe hati zao za kusafiria mahakamani, wasitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama na hawaruhusiwi kufanya mkutano wowote ule unaohusiana na mambo ya DECI.

No comments:

Post a Comment