.

.

.

.

Saturday, September 19, 2009

SPIKA WA BUNGE APETA DHIDI YA CHAMA CHAKE

WAKATI Spika Samuel Sitta ameeleza kushangazwa na kitendo cha katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kummwagia sifa kemkem akiwa jimboni kwake Urambo Mashariki, chama hicho tawala kinaonekana kusalimu amri kwa kiongozi huyo wa Bunge la Jamhuri.
Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) ilitoa kali iliyoonekana kulenga kuwadhibiti wabunge wa chama hicho wanaojinadi kuwa vinara wa vita ya ufisadi, baada ya kikao chake ambacho imeelezwa kuwa kilimbana Spika Sitta kwa madai kuwa anaruhsu mijadala inayokichafua chama na serikali yake.
Sitta pia alituhumiwa kuwa anapendelea kikundi cha wabunge wachache ambao wamekuwa wakitoa tuhuma mbalimbali za ufisadi dhidi ya wanachama wa CCM na serikali, tamko lililosababisha kikundi cha wabunge hao kuanza kutoa taarifa kuwa hakitakubali kufungwa mdomo kwa kuwa vita yao ni takatifu.
Hata hivyo katikati ya wiki, Makamba alisafiri hadi Tabora na kwenda Urambo Mashariki ambako alihutubia mkutano wa hadhara na kummwagia sifa Sitta, huku akisema kuwa yeye binafsi wala CCM hawana ugomvi na mbunge huyo, kauli ambayo imemshangaza hata mwenyeji wake.
Hata hivyo, Sitta alisema anaamini kuwa kamati ya rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambayo iliundwa kuchunguza misuguano baina ya wabunge na wanachama wa CCM na inayotarajiwa kutoa ripoti yake hivi karibuni, itamaliza mzizi wa fitina.
"Unajua mimi binafsi nashangaa tu ndugu yangu, lakini kamati ya akina Mzee Mwinyi itafanya kazi yake na ukweli utakuwa wazi," alisema Sitta.
Akizungumza kwa makini huku akiwa hataki kuingia kwa undani kwenye suala hilo, Sitta alisema baada ya kamati hiyo kutoa majibu yake, atakuwa huru zaidi kuzungumzia sakata hilo.
Alipoulizwa kama haoni kuwa hizo zinaweza kuwa njama za wabaya wake kumsogeza karibu nao ili wammalize, Sitta alisema: "Sifikirii kitu kama hicho kuwa kinawezekana.
"Aah nafikiri hatutakiwi kufika huko kwa kutoa tafsiri hizo, kikubwa tuipe muda kamati ifanye kazi yake."
Sitta hakutaka hata kuzungumzia sifa alizomwagiwa na Makamba ambaye ni mbunge wa kuteuliwa.

Mabadiliko ya ghafla ya viongozi wa CCM dhidi ya Sitta na kundi linalojinadi kuwa ni vinara wa vita ya ufisadi, yamekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wabunge waendelee kuikosoa serikali.
Rais Kikwete alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi kwa staili mpya ya mazungumzo ya moja kwa moja kwa njia ya simu na ujumbe mfupi wa simu na barua pepe akitumia redio na televisheni.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ambaye alisimamia kikao cha Nec ambacho inadaiwa kuwa kilimbana Sitta, imeelezwa kuwa imetolewa kwa lengo la kuweka mambo sawa baada ya wabunge kurushiana maneno makali kwenye kikao hicho kilichofanyika Dodoma.
Kikao hicho pia kilipitisha kwa kauli moja uamuzi wa kuunda kamati ya watu watatu chini ya rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kuwachunguza wabunge wenye tabia hiyo na kuwachukulia hatua ambayo tayari Nec imependekeza kuwa ni kuwaondoa kwenye nyadhifa zao ama kuwafukuza uanachama.
Ilielezwa kuwa wajumbe 22 waliochangia hoja hiyo walitaka spika wa Bunge, Samuel Sitta anyang'anywe kadi ya CCM kwa kile walichodai kuwa ni mtu hatari aliyejeruhiwa na ambaye akiendelea kuachwa atakiweka chama pabaya.
Badala ya kumfukuza Sitta, Nec ilikubaliana kuunda kamati ya watu watatu ambao ni Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, spika wa zamani, Pius Msekwa na waziri wa zamani, Abrahaman Kinana kwa ajili ya kuangalia kwanini hali ya kutoelewana imejitokeza ndani ya CCM, serikali na Bunge.
Akizungumza baada ya kikao hicho cha Nec, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati aliwaambia waandishi wa habari Nec imeamua kuunda kamati maalum ya kuwashughulikia wabunge wake wanaoikosoa serikali ya chama hicho tawala, huku ikimuwekea kinga rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Alidai bunge limeanza kuwa kama mchezo wa (kikundi cha televisheni cha vichekesho) Ze Comedy kutokana na kila mtu kufanya mambo yake mwenyewe hali ambayo inaweza kusababisha watu kurushiana hata viatu ndani ya ukumbi wa bunge.
Alionya kuwa hali hiyo sasa inatosha na kwamba walipofikia panatosha wasiendelee mbele.
"Wanaoropoka hovyo ni walevi na tumeona kuna kundi dogo ambalo limejiona kama ni wateule wa kuzungumzia ufisadi bila ya kujua wabunge wote wana haki ya kuzungumzia suala hilo," alisema Chiligati.
Maelezo hayo ya Chiligati yaliwekewa msisitizo na tangazo lililotolewa katika gazeti la chama hicho likisisitiza kuwaziba midomo wabunge ambao mapambano yao ya ufisadi yanakichafua chama na serikali.
Hata hivyo, wiki hii Chiligati alibadili ghafla msimamo huo na kuwahamasisha wabunge wapambanaji wa ufisadi nchini kuendeleza mapambano, huku ziara ya Makamba kwenye Jimbo la Urambo Mashariki ikitoa picha mpya ya msimamo wa CCM.
Akitoa maoni yake kuhusu kubadilika huko kwa ghafla, mbunge wa Maswa, John Shibuda aliwafananisha Makamba na Chiligati na walokole ambao hubadilika imani baada ya kuhubiriwa na kukiri makosa.
Shibuda alisema Spika Sitta alikuwa sadaka ya kafara ambayo ilisaidia wana-CCM wote kupata uhuru.
"Fedheha zote zilizomkuta Sitta ni sawa na damu ya mwanakondoo msalabani, fedheha aliyopata Spika Sitta imegeuka ukombozi na sasa CCM imepata walokole waliobadilika, baada ya kuamini mahubiri waliyopewa na timu iliyokuwa ikipinga dhuluma na vitendo visivyozingatia utawala bora,” alisema Shibuda.
Alisema awali kikundi kidogo cha mafisadi kilitumia watu kutaka umma uone kuwa Bunge sio sauti ya umma, lakini baada ya mahubiri ya wateule hao wanaozunguka maeneo mbalimbali, sasa wametambua kuwa bunge halina itikadi ya chama wala makabila na badala yake viongozi wote wanawajibika kwa katiba ya nchi.
Shibuda alimpongeza Rais Kikwete kwa kusimamia haki kwa mujibu wa katiba ya nchi na kwamba ametumia ustaarabu wa kutopenda ugomvi na kutoa uhuru kwa watu kuzungumza na kutofautiana kwa hoja bila kupigana.
Akiwa Tabora, Makamba alimsifia Spika Sitta na kuhamasisha mapambano dhidi ya ufsadi.
Katika kile kinachoonekana kugeuka kwa CCM, mtendaji huyo mkuu wa chama alisema CCM ipo pamoja naye katika kutekeleza majukumu yake kama spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Makamba alimmwagia Sitta sifa hizo alipokuwa akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa CCM wilaya ya Urambo.
Alisema Sitta ni mtu muelewa, asiyetetereka na wala kuyumbishwa na mtu yeyote na kwamba anachokifanya ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Inaonekana kugeuka huko kunaweza kuwa kumesababishwa na msimamo wa nchi wahisani ambazo zilihoji uhalali wa kumbana spika na wabunge wanaopambana na ufisadi katika kikao kilichopita cha Nec.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa kitendo cha wahisani kuhoji na kuzuia kiasi cha msaada, wakitaka kupata maelezo ya kina kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya kampuni ya Kagoda Agricultural Limited inayodaiwa kuchota Sh bilioni 40 kutoka BoT, kinaweza kuwa sababu ya mabadiliko hayo ya ghafla ya msimamo ndani ya CCM.
Tayari CCM imewaandikia barua wahisani ikitetea maamuzi ya Nec, huku ikikiri kumbana spika na kufafanua kuwa hatua hiyo ilifikiwa kutokana na Sitta kuwa mwanachama wa CCM.
Wakati baadhi ya wachambuzi wakiona kugeuka huko kwa ghafla ni sawa na CCM kuokoka kutoka katika madhambi yake, wengine wanaona kuwa hizo ni mbinu za mafisadi ndani ya chama hicho kuunda mkakati mpya wa falsafa ya 'mpende adui yako' ikiwa ni njia nyingine ya kummaliza mbunge huyo wa Urambo Masharikii.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, mkurugenzi wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Fordia, Buberwa Kaiza alisema CCM inaonyesha walakini katika uongozi wake na ni dhahiri kuwa hawauwezi uongozi.
Alisema hatua za jumuiya za kimataifa zikiwemo balozi za nje kuonyesha kukerwa na kitendo cha CCM kumbana spika, ni aibu na ishara ya chama kuonyesha upungufu katika uongozi.
Alisema kitendo cha Nec kujaribu kubadilisha bunge liwe linalokidhi matakwa ya kundi dogo lisilozingatia maadili katika uongozi, kinaonyesha kuwa chama hicho hakijali maslahi ya wananchi badala yake ni wakala wa watu wachache wasiolitakia mema taifa hili.
Naye mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, John Mgeja aliipongeza kazi inayofanywa na wabunge wanaopinga ufisadi, lakini akawakumbusha kuwa nchi ina utawala wa sheria na waeleze ukweli kwa kuwa ndicho ambacho wananchi wanahitaji.
Mgeja alisema suala la kupambana na ufisadi si jambo jipya ndani ya CCM na kwamba ni sera ya chama hicho iliyokuwepo tangu enzi za TANU na Afroshiraz.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveri Lwaitama aliupongeza uamuzi wa viongozi wa juu wa CCM na akasema ni ishara kuwa wamegundua wanachama wao waliokuwa wakipinga ufisadi wanakitakia mema chama hicho.
"Inavyoonekana CCM wameanza kuwaelewa kina (mbunge wa Kyela, Harrison) Mwakyembe, (mbunge wa Nzega, Lucas) Selelii na (mbunge wa Same Mashariki) Anna Kilango. Wamegundua wabunge hawa wanakitakia mema chama chao na ndio sababu wameamua kuwaunga mkono," alisema Dk. Lwaitama.
Dk. Lwaitama alisema inavyoonekana mapambano yaliyoanzishwa na wabunge hao yameonekana kuipatia sifa CCM ingawa alisema kwa upande wake anapata shida kuelewa endapo maamuzi hayo ni mchezo wa kuigiza au mikakati ya kweli.
Baadhi ya watu pia wanakitafrisi kitendo cha mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kutamka hadharani kwa uwazi kwamba hajafikiria wala kutangaza kokote kuwa ana mpango wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010, kuwa ni mabadiliko makubwa ndani ya CCM.
Lowassa, ambaye alilazimika kujiuzulu uwaziri mkuu baada ya kutajwa kwenye kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development (LDC), wiki hii alisema wazi kuwa hakuna mtu ambaye anaweza kumtenganisha na Kikwete katika urafiki wao kwa sababu hawakukutana barabarani.
Mwaka 2005, Lowassa hakuingia kwenye mbio za urais ndani ya CCM kutokana na kile kilichoonekana kuwa ni kumwachia Kikwete lakini, tangu aachie uwaziri mkuu amekuwa akichukuliwa kama mtu ambaye anaweza kupambana na rafiki huyo mkubwa kuwania urais mwaka 2010 kwa tiketi ya CCM.

No comments:

Post a Comment