KITENGO cha Hija kinachoshughulikia safari za mahujaji wa Tanzania, watakaokwenda kuhiji katika miji mitakatifu ya Mecca na Madina, Saudi Arabia mwaka huu, kimetangaza masharti mapya yaliyotolewa na serikali ya nchi hiyo, kwa mahujaji.
Masharti hayo yanahusu makundi matatu ya watu ambao hawataruhusiwa kwenda nchini humo, kuhiji.
Makundi hayo ni ya watoto wa umri wa chini ya miaka 12, watu wa umri zaidi ya miaka 65, wanawake wajawazito na watu ambao joto lao mwilini, linazidi nyuzi joto 38.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kaimu mwenyekiti wa kitengo hicho, Shehe Khalid Mohamed alisema, masharti hayo yametolewa na serikali ya Saudi Arabia.
Alisema kitengo chake kimeshapokea waraka kutoka katika Ubalozi wa Saud Arabia hapa nchini, ukiwataka mahujaji kufuata masharti hayo.
Alisema lengo la kukataza makundi hayo kwenda kuhiji, ni kudhibiti kuingiza kwa homa ya mafua ya nguruwe katika nchi hiyo.
Alisema, kwa mujibu wa waraka huo, makundi yaliyozuiliwa kwenda hija, ni rahisi kuambukizwa homa ya mafua ya nguruwe.
Pia alisema joto la kiwango cha juu cha nyuzi joto 38 ni moja ya dalili ya homa hiyo na kwamba yeyote atakayekuwa na kiwango hicho cha joto hatapata viza ya kumwezesha kuingia Saudi Arabia.
"Hakuna mtu atakayepewa viza bila kupimwa homa ya manjano na mafua ya nguruwe, hii inatokana na hofu ya ugonjwa huu iliyotanda duniani kwa sasa, tumeshayapa taarifa hizi makampuni yote yanayohusika katika kusafirisha mahujaji," alisema Shehe Mohamed.
Shehe Mohamed aliwasihi Waislamu wenye umri wa chini ya miaka 12 na zaidi ya 65 kuahirisha safari kwa mwaka huu.
"Nawataka Waislamu wenye tabia ya kwenda kwa daktari na kusainiwa vyeti kuwa afya ziko safi waache kwa sababua masharti ya mwaka huu ni makali,"alisema Shehe Mohamed.
Kuhusu maandalizi ya safari, Shehe Mohamed alisema hadi sasa ni taasisi tatu tu zilizofikisha 50% ya malengo kati ya taasisi 14 zinazojihusisha na usafirishaji wa mahujaji.
Alisema Tanzania imepewa nafasi ya kupeleka mahujaji 25,00 katika hija ya mwaka huu.
Alisema mashariti yaliyotolewa na Saudi Arabia yatachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya watu watakao kwenda kuhiji katika mwaka huu.
Alisema sababu nyingine itakayo athiri safari ya mwaka huu ni mtikisiko wa uchumi duniani.
"Watu wengi walikuwa wanategemea kusafirishwa na watoto wao walio nje ya nchi, lakini mtikisiko wa uchumi duniani umewaathiri kwa hiyo nayo hiyo ni sababu moja wapo itakayoathiri safari ya mwaka huu," alisema She Mohamed.
Kila mwaka zaidi ya Waislamu milioni tatu duniani hukusanyika katika miji ya Mecca na Madina, kwa ibada ya hija .
Wakati Tanzania ikikubali kwa kauli moja kufuata mashariti yaliyotolewa na Saud Arabia kuhusu ibada hiyo, Kenya kumewa na mgawanyiko huku kundi moja likikubali kufuata mashariti na lingine likisema huo ni ukandamizaji.
Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Nation la Kenya toleo la Septemba 23, viongozi wa dini wamesema sheria hizo zinalenga katika kuwakandamiza wazee na wanawake.
No comments:
Post a Comment