Kijana Thomas Peter, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25-30 amekutwa amekufa huku kichwa chake kikiwa kimetobolewa na macho kutolewa na watu wasiofahamika.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo katika maeneo ya makaburi ya Mande, Mbagala Mgeninani.
Afisa usalama wa Umoja wa Waendesha Pikipiki Mbagala Mgeninani, Ismail Mweri, amesema wamesikitishwa na kifo hicho na kuliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wahusika.
Akizungumzia kuhusiana na tukio hilo, afisa usalama huyo amesema marehemu alikodiwa na mtu mmoja saa 4 usiku akitaka kupelekwa ya Mande.
Inadaiwa kuwa baada marehemu kufika huko alifanyiwa unyama huo na kisha watuhumiwa kutoroka na pikipiki hiyo.
Amedai kuwa baada ya kubaini marehemu amekaa muda mrefu bila ya kurudi walianza kumfuatilia ndipo alfajiri waliweza kuukuta mwili wa marehemu katika maeneo ya makaburi ya Mande huku akiwa amepasuliwa kichwa na kutobolewa macho.
“Tulimkuta marehemu kichwa chake kikiwa kimepasuliwa na macho yake kutolewa na pia katika sehemu mbalimbali za mwili wake kukiwa na majeraha mbalimbali,” amedai kiongozi huyo.
Amedai kuwa mbali ya kuwapo kwa tukio hilo pia mwendesha pikipiki mwingine amenusurika kufa baada ya kukodiwa na mtu mmoja aliyetaka kupelekwa katika maeneo hayo ya makaburi.
Amedai kuwa wakati anamshusha mteja huyo ghafla walitokea vijana wawili waliomkaba na kisha kumpiga na kitu kikali kichwani huku wengine wakimfunga kamba lakini aliweza kuwatoroka.
Kutokana na hali hiyo mwendesha pikipiki huyo aliamua kupiga kelele kuwa ameibiwa pikipiki yake ndipo wasamaria wema, kwa kushirikiana na madereva wenzake, waliendesha msako katika makaburi hayo na kufanikiwa kuikuta pikipiki ikiwa imefichwa.
“Tuliikuta pikipiki imefichwa chini ya gogo na tulifanya msako lakini hatukuweza kuwabaini wahusika,” amedai kiongozi huyo.
Hata hivyo, amesema kuwa operesheni hiyo iliendelea usiku kucha na waliweza kumkatama kijana mmoja ambaye alikiri kuhusika na tukio hilo.
“Tulipomuuliza alikiri lakini wakati tunaendelea na mahojiano akakimbia, hapo ndipo alipoamsha hasira za watu. Walimkimbiza na kisha kumpiga hadi kumuua,” amedai.
Amesema kutokana na matukio hayo hivi sasa dereva mwingine hajulikani aliko wala pikipiki yake na tayari wametoa taarifa katika kituo cha polisi Mbagala na wanaendelea na jitihada za kumtafuta.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Liberatus Sabasi, hakuweza kupatikana kuzungumzia zaidi tukio hilo.
No comments:
Post a Comment