.
.
Friday, May 07, 2021
RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA WAZEE WA DAR ES SALAAM
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
RAIS wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wazee wote nchini kwamba masuala yote yanayohusu wazee yatashughulikiwa kwa nguvu zote ikiwemo ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Akizungumza leo mbele ya wazee hao wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya wazee wa nchi nzima, Rais Samia ametumia nafasi hiyo kufafanua mambo yanayohusu wazee kwa kina huku akiahidi yote ambayo yamezungumzwa na wazee hao kwenye risala yao ni ya msingi na lazima yafanywie kazi kadri itakavyooekana inafaa.
Rais Samia amesema kuna mambo amboyo ya kisera kuhusu wazee ambayo amewahakikishia katika maboresho ya sera yanaendelea kufanywa kwa sasa na watatumia nafasi hiyo kuangalia sera zinazohusu wazee ili ziweze kuboreshwa na kuwa na tija.
"Haya ambayo mmesema wazee wetu nayo watatupia macho, shida ambazo mnazipata na wigo wa kupanua matibabu tunakwenda kufanyia kazi, lakini niseme si mara ya kwanza kusikia, mikoani huko wazee wanalalamikia haya haya, na ukisikia mtu mzima analia ujue kuna jambo, hivyo tutafanyia kazi.
"Suala lingine ambalo mmelizungumza ni kuhusu afya ya wazee, na hili la afya kwa wazee limezungumzwa vizuri kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo kwa vyovyote vile sina jinsi ya kulikimbia, tutashughulikia masuala yote ya afya ya wazee.
"Na hapa natoa maagizo kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto akasimamie haya leo na si kesho.Tunatambua dunia iko kwenye janga la Corona na wanaoathirika zaidi ni wazee, hivyo nataka nitoe taarifa kwa wazee, Kamati ambayo nimeiunda itatoa taarifa.
"Hivyo yale yote ambayo yanasababisha wazee kuwa hatarini zaidi tutahakikisha tunayafanyia kazi, na tutawalinda, na tutawaelekeza wazee namna ya kujilinda.Masuala yote yanayohusu wazee tutayaweka vizuri, ,"amesema Rais Samia.
Amesisitiza," Sisi wote ni wazee na mimi nimeingia kwenye umri wa uzee, hivyo lazima tuweke mambo haya vizuri, ili nami yasije kunikuta.Kwa hiyo na mimi itabidi nirekebishe masuala ya wazee mapema ili nikija huko nikute mambo yako vizuri".
Aidha kwenye eneo la uchumi , Rais Samia amesema anakubaliana na wazee lakini kama alivyotangulia kueleza Waziri wa Afya Dk.Doroth Gwajima watangalia namna ya kushughulikia."Kupitia mfuko wa TASAF tumekuwa tukisaidia kaya masikini, na hivyo tunaangalia uwezekano wa wazee wote kuingia kwenye mfuko huo.
"Na tunandaa mfuko mwingine unaofaa na huo ambao wazee wataingia humo.Pia kuna wazee ambao wamelitumikia Taifa na serikali imekuwa inatoa pensheni kwa ajili yao, lakini kuna hili ambalo limezungumzwa la pensheni kwa wote.
"Serikali ilijadili hili lakini tukaona utekelezaji wake ni mgumu, kulingana na bajeti ya Serikali, wazee wako karibu milioni 2.5, hivyo tuliamua kuanza na wazee wenye umri wa miaka 70, na kwa hali ilivyo sasa uchumi umeshuka.Uchumi wa Tanzania umeshuka kutoka asilimia saba wa ukuaji hadi asilimia tano.
"Na tuna miradi mikubwa ambayo tunaendelea nayo , hivvyo naomba niseme hili la pensheni kwa wote tuliache kwanza ili tumalizie miradi tuliyonayo, tunatamani tutoe hata Sh.30,000,lakini hatutaweza.Watumishi wa umma hajapandishiwa mshara kwa miaka mitano tano sasa,"amesema Rais Samia.
Kuhusu uwakilishi wa wazee katika Baraza la Madiwani na Bungeni hilo ni muhimu kuwa na wazee kwenye vyombo vya hivyo ili kuwa na uwakilishi wao."Hata hivyo kwa kutambua yote haya kuna fursa ambazo tumezitoa kwa wazee.
"Nipongeze Chama changu cha CCM wazee wametambuliwa na wapo kwenye mfumo. Hata hivyo nafasi ya wazee iko kwenye umoja wa wazazi hivyo ni vema wakashikamana na jumuiya ya wazazi lakini huko mbele ya safari tutaona namna ya kufanya ili wazee wawemo,"amesema Rais Samia.
CREDIT: Michuzi blog
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment