.

.

.

.

Monday, March 22, 2010

BENKI KUU TATU ZALIZWA MABILIONI YA SHILLINGI

WATU wasiofahamika wameghushi nyaraka za malipo na kuiba zaidi ya Sh300 bilioni katika benki tatu kubwa nchini na kusababisha mtikisiko mkubwa katika sekta ya fedha, uchunguzi umeonyesha.

Kwa mujibu wa uchunguzi , fedha hizo ziliibwa mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni kabisa mwa mwaka huu, kwa njia ya mtandao wa kompyuta na kuhusisha wezi wa kimataifa ndani na nje ya nchi.

Tukio hilo ambalo ni kubwa kuwahi kutikisa sekta ya fedha nchini tangu uhuru mwaka 1961, limetokea katika kipindi cha takribani miaka miwili tangu serikali ianzishe kitengo maalumu cha Intelejensia cha kufuatilia Mzunguko wa Fedha chafu (FIU).

Licha ya kuwepo FIU, ambayo iliundwa pamoja na Sheria ya Kupambana na Fedha Chafu ya mwaka 2007, uchunguzi wa Mwananchi, umebaini kutokea wizi huo mkubwa katika benki hizo.

Uchunguzi huo umebaini kwamba, taarifa za awali zinaonyesha fedha hizo ambazo ni mara tatu ya zile za EPA zilizoibwa katika Benki Kuu Tanzania (BoT), zilihamishwa kwa njia ya kompyuta kwa kughushi malipo kwenda kwa wahusika wa mtandao huo katika nchi za Hong Kong, Uingereza na Marekani ambako Polisi wa Kimataifa wa nchini na wenzao wanahaha kuzichunguza.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, alipoulizwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, alithibitisha kuwepo taarifa za uhalifu huo, lakini akaweka bayana, hakuna ushahidi wa kiwango maalumu kilichoibwa hadi sasa.

"Hizo taarifa zipo zinafanyiwa kazi, ila haijathibitika ni kiasi gani cha fedha kimeibwa na benki zipi hasa, kwa hiyo kusema ni Sh300 bilioni au zaidi ya hapo, si sahihi hakuna uthibitisho wowote," alifafanua DCI Kamishna Manumba.

DCI Manumba aliongeza kwamba, baada ya uchunguzi kukamilika polisi itatoa taarifa za kina, sahihi na kwa wakati kwa wananchi na kusisitiza, "Kwa sasa ngoja tufanye kazi."

Hata hivyo, DCI Manumba alionya na kuzitaka benki na watu wengine kuwa makini katika kuangalia usalama wa mali na fedha katika kipindi chote.

"Unajua, mambo ya uhalifu sisi tunajitahidi kukabiliana nayo lakini bado wengine wanaendelea kwa kutumia mbinu mbalimbali. Kwa mfano tunazuia watu wasibakwe, lakini wanabakwa, hii yote inaonyesha umuhimu wa watu kuwa makini," alifafanua DCI Manumba.

Gavana wa Benki Kuu (BoT) Profesa Benno Ndulu, alipoulizwa kuhusu sakata hilo alisema yuko nje ya nchi kikazi.

"Niko Sweden kikazi, halafu hapa siwezi kukusikia vizuri wala kuzungumza vema kwani kuna shughuli ambayo nimehudhuria," alisema Profesa Ndulu, ambaye taasisi kuu ya fedha ya nchi ina wajibu wa kusimamia benki na taasisi zote za fedha nchini.

Baadhi ya maofisa wa benki hizo ambazo majina yake tunayahifadhi, wamethibitisha kukumbwa na uhalifu huo mkubwa na kwamba wameacha suala hilo mikononi mwa vyombo vya dola.

"Ni kweli kuna vitenfo vya kughushi vimetokea katika benki yetu, lakini hilo hatuwezi kulizungumzia kwa kina kwasababu liko mikononi mwa vyombo vya dola. Polisi wanaweza kulizungumzia hilo," alifafanua ofisa kutoka moja ya benki iliyoibiwa kiasi kikubwa cha fedha karibu Sh100 bilioni.

Wakati DCI Kamishna Manumba, Gavana Ndulu na maofisa wa benki wakizungumzia hayo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba, fedha hizo ziliibwa mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni kabisa mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, hadi sasa taarifa za awali zinaonyesha mpango huo mchafu umeanzia ndani ya benki kwa kuhusisha baadhi ya watu ambao ni wanamtandao na wezi wenzao nje ya nchi.

Mwananchi imebaini kwamba, hadi sasa Idara ya Interpol Tanzania kwa kushirikiana na wenzao wa nje wanafanya uchunguzi huo wa kina katika nchi za Hong Kong, Uingereza na Marekani ambako taarifa za awali zinaonyesha fedha hizo zilikwenda.

Katika uchunguzi huo, imebainika kwamba baada ya mpango huo kufanywa nchini fedha hizo zinaonyesha zilihamishwa kwa njia hiyo ya kughushi kwenda nchi hizo.

Vyanzo hivyo vya habari za kiuchunguzi, zilifafanua kwamba baadhi ya watu katika mabenki hayo ambao wanafahamu mzunguko wa fedha ikiwemo malipo ya ndani na nje, wamepanga njama hizo na kughushi malipo kwa kushirikiana na mtandao mkubwa wa wezi wenzao wa nje ya mabenki ndani na nje.

Habari hizo za kiuchunguzi, zinaonyesha kwamba wizi huo umetikisa mabenki hayo kiuchumi huku duru za kiusalama zikisema vyombo vya usalama vimekuwa makini kuangalia fedha hizo zimeingia mikononi mwa watu gani.

Imebainika kwamba, kiasi hicho kikubwa cha fedha kinaweza kuweka usalama wa taifa hatarini endapo kitakuwa kimeingia kwenye mikono ya watu ambao wana nia mbaya na nchi.

"Ni kiasi kikubwa cha fedha, kama kitakuwa kimeingia kwenye mikono ya watu hatari wanaweza kuhatarisha usalama wa nchi, bilioni 300 si kitu kidogo," kilisema chanzo kimoja kutoka moja ya vyombo vya usalama.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kitisho kingine kinachoangaliwa hadi sasa ni iwapo fedha hizo zimeibwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba kwa ajili ya kundi fulani ikiwemo mafisadi kutaka kuzitumia kutimiza malengo yao.

"Tunaangalia pia, maana inawezekana ni mafisadi wakubwa ambao wanajua mzunguko wa fedha ndiyo wamekula njama na kutaka kuhujumu nchi kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu," kilifafanua chanzo hicho.

Ingawa haijathibitika, lakini kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kuliibuka ufisadi mkubwa katika BoT ambao zaidi ya Sh 133 bilioni ziliibwa.

No comments:

Post a Comment