MWANAMKE ambaye ni mke wa mtu mwenye watoto watatu, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mapenzi na mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 15.
Mbali na mwanamke huyo, Sophia Philemon (44) mkazi wa kambi namba tisa katika kiwanda cha sukari cha TPC, wilaya ya Moshi vijijini kuhukumiwa kifungo hicho, pia ameamriwa kumlipa mwanafunzi huyo fidia ya Sh1 milioni.
Hukumu hiyo, ilitolewa jana mjini Moshi na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Kilimanjaro, John Nkwabi baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashitaka.
Nkwabi alisema ushahidi wa mashahidi hao, akiwemo mwanafunzi huyo wa sekondari ya Langasani, umeithibitishia mahakama pasipo shaka yoyote kwamba mwanamke huyo, alimlazimisha mtoto huyo kufanya naye tendo la ndoa.
Kitendo hicho ni kosa chini ya kifungu namba 138B (1) (d) cha kanuni ya adhabu kinachosimamia makosa ya kimapenzi kwa watoto baada ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hakimu Nkwabi alisema mahakama imeridhika na ushahidi kuwa Februari 28, mwaka jana, saa 1:00 usiku huko kambi namba tisa, mshitakiwa alimlazimisha mwanafunzi huyo kufanya naye mapenzi katika chumba anachoishi na mumewe.
Muda huo, mwanafunzi huyo alikuwa ametoka dukani alikokuwa ametumwa na wazazi wake na mwanamke huyo, alimwita na kumshawishi aingie ndani ya nyumba yake na baadaye kumlazimisha kufanya naye tendo la ndoa.
Baada ya kutiwa hatiani, wakili wa serikali, Hellen Moshi aliyeendesha kesi hiyo, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwani vitendo vya ubakaji vinazidi kuongezeka nchini hususan kwa watoto wadogo na wanafunzi.
Katika utetezi wake, Sophia alisema ni mke wa mtu na hakubahatika kupata mtoto na mwanaume huyo, lakini kabla kuolewa alikuwa tayari amezaa watoto watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume.
Mshitakiwa alikuwa alikataa kufanya tendo la ndoa na mtoto huyo, licha ya kumfahamu kuwa ni jirani yake. Utetezi wake ulitupiliwa mbali na mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment