.

.

.

.

Friday, March 19, 2010

MGAO WA UMEME TENA !!!

SHIRIKA la Umeme (Tanesco), ambalo mwishoni mwa mwaka jana lilisema kuwa suala la mgawo wa umeme sasa ni historia, jana limetangaza kuanza kwa mgao kwenye mikoa yote kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa umeme kwenye baadhi ya vituo vya uzalishaji.

Baada ya mafundi kufanikiwa kutengeneza mtambo wa megawati 40 ambao pamoja na kuharibika kwa mitambo kwenye mabwa ya Kihansi na Hale ulisababisha mgawo mkubwa wa umeme, Tanesco ilisema tatizo hilo la umeme sasa ni historia labda iwe dharura.

Lakini jana ilikuwa na taarifa nyingine iliyotolewa na kaimu mkurugenzi mtendaji wa Tanesco, Stephene Mabadaikielezea kurejea tena kwa mgawo kunakotokana na kupungua kwa uzalishaji wa umeme kwenye vituo vya Kidatu, Kihansi, Pangani na Ubungo.

Kwa mujibu taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, mgawohuo unataanza wakati wowote kwenye baadhi ya maeneo na watumiaji wataukosa kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 4:00 usiku wakati Tanesco ikiendelea na taratibu za kurudisha umeme katika hali ya kawaida.

Taarifa hiyo imesema kuwa pamoja na mgawo huo, shirika hilo linakabiliwa na tatizo la uharibifu wa baadhi ya mitambo yake ambayo mingi ni michakavu na kwamba inafanya juhudi kumaliza matatizo hayo.

Hata hivyo, kabla ya Tanesco kutangaza rasmi mgawo huo, tayari baadhi ya maeneo yalishaanza kuonja adha ya kukosa nishati bila ya kupata maelezo sahihi ya tatizo hilo.

Kukosekana huko kwa umeme kumeelezewa kuwa kunasababisha uharibifu wa mali na bidhaa ambazo huhifadhiwa kwa kutumia nguvu ya nishati hiyo.

“Sisi huku tuna mgawo usiokuwa na taarifa... hali hii imetuathiri kwani mgao hauna ratiba maalum. Muda wowote umeme unakatika na kurudi kwa kipindi kifupi na kusababisha baadhi ya vifaa vyetu kuharibika,alisema mkazi wa Kurasini, Mussa Mohamedi.

Hata hivyo, katika taarifa yake ya jana Tanesco imeomba radhi wateja wake kutokana na hali hiyo iliyosema imekuwa kikwazo kikubwa wa watumiaji.

No comments:

Post a Comment