KINYANG’ANYIRO cha kumpata Spika mpya wa Bunge kitafikia tamati wiki hii wakati wabunge wateule watakapopiga kura kumchagua Spika huyo na kuapishwa tayari kuanza rasmi shughuli za Bunge.
Spika huyo atakayepatikana Ijumaa wiki hii baada ya kuanza kwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge mjini Dodoma ambao utatanguliwa na wabunge kujisajili kuanzia leo.
Akitoa ratiba ya mkutano huo Dar es Salaam jana, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah alisema kinyang’anyiro hicho kitaanza keshokutwa kwa kila chama cha siasa kilichosajiliwa kinachokusudia kushiriki katika uchaguzi wa Spika kuwasilisha kwake, jina moja la mgombea wake wa nafasi hiyo.
Alisema kila chama kinaruhusiwa kumpendekeza mgombea ambaye si mbunge ili kugombea nafasi hiyo na kinapaswa kuwasilisha jina la mgombea wake kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi siku tano kabla ya siku ya uchaguzi wa Spika ili Tume ijiridhishe iwapo mgombea huyo anakidhi au hakidhi matakwa ya masharti.
Alisema siku mbili kabla ya uchaguzi, NEC itawasilisha majina ya wagombea wa nafasi hiyo wenye sifa huku wabunge wanaotaka kugombea nafasi hiyo, mgombea au Katibu wa chama atawasilisha jina la mgombea katika Ofisi ya Katibu wa Bunge si zaidi ya saa 10 jioni siku ya uteuzi.
Hadi sasa, waliotangaza rasmi kugombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni Mbunge Mteule wa Urambo Mashariki, na Spika aliyepita, Samuel Sitta; Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge; Anne Makinda, ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Tisa;
Mbunge Mteule Anna Abdallah; Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Kate Kamba na Job Ndugai ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge lililomaliza muda wake.
Wengine ni Mhasibu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Stephen Deya; Mjumbe wa Baraza la Vijana Mkoa wa Pwani, Mohammed Nyundo; Benedict Lukwembe; Mwalimu wa Sekondari ya Tambaza, Salum Kingulilo; Peter Nyalali aliyechukua fomu jana na Mwandishi wa Habari, Kazimbaya Makwega.
Mbunge Mteule wa Peramiho, Jenista Mhagama amejitosa kuwania kuwa Naibu Spika.
Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi CCM, Matson Chizii alisema Kamati Kuu itakutana kesho kuchambua majina ya wagombea na kuchagua matatu yatakayopelekwa katika Kamati ya Wabunge wa chama hicho itakayoteua jina moja.
Katibu wa Bunge alisema baada ya kumpata Spika, kuanzia Ijumaa hadi Jumanne wabunge wataapishwa na siku hiyo mchana, jina la Waziri Mkuu litatangazwa ili lithibitishwe.
Alisema endapo Sikukuu ya Idd El Adha itakuwa Novemba 15 au 16, Bunge litasitisha shughuli zake hadi siku inayofuata.
Jumatano ijayo asubuhi, Waziri Mkuu ataapishwa katika Ikulu Ndogo ya Chamwino na baadaye jioni Rais Jakaya Kikwete atalihutubia Bunge kisha Bunge kuahirishwa
No comments:
Post a Comment