.

.

.

.

Friday, September 23, 2011

TANESCO YASEMA ATI .................


MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), William Mhando amesema makali ya mgawo wa umeme yatapungua mwanzoni mwa mwezi ujao baada ya Kampuni ya Aggreko kuingiza megawati 100 za umeme katika Gridi ya Taifa.

Mhando alisema tayari kampuni hiyo imeingiza megawati 22 huku Kampuni ya Symbion ikiwa imeingiza megawati 35 za umeme katika Gridi ya Taifa.

Akizungumza wakati wa mkutano na wadau wa nishati na madini kujadiliana kuhusu
utekelezaji wa mipango ya Serikali ya mwaka 2010 na 2011, alisema megawati hizo 100 za Aggreko zitaingia kwenye Gridi ya Taifa, Oktoba 10, mwaka huu.

Pia alisema tatizo la mgawo wa umeme litadhibitiwa zaidi baada ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuingiza megawati 50 za umeme katika gridi hiyo mwanzoni mwa mwezi ujao.

Mhando alisema megawati 205 zinazotakiwa kuzalishwa na Kampuni ya Symbion ambayo Serikali imeingia nayo mkataba kwa kushirikiana na Tanesco na Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura), ziko katika hali nzuri nazo kuzalisha umeme.

Akizungumzia umeme wa kutumia upepo, alisema Kampuni ya Wind East Africa Ltd, tayari imeanza mazungumzo ili kufikia makubaliano ya bei na wameomba Benki ya Dunia kusaidia kutoa ushauri.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi akifungua mkutano huo, alisema katika mipango ya Serikali watahakikisha kuwa wanapata megawati 572 walizoahidi baada ya kampuni hizo kuzalisha umeme na kuingiza katika gridi ya taifa kwa awamu.

CHANZO: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment