.

.

.

.

Sunday, May 27, 2012

AOKOA MAELFU TAZARA ......

KATIKA tukio lisilo la kawaida, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, juzi usiku alivamia katika Stesheni za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwanusuru abiria waliokwama kwa zaidi ya saa 12 katika stesheni kuu hiyo. 

Abiria hao, wakiwemo wagonjwa na watoto, walikuwa wanasafiri na treni ya mamlaka hiyo kwenda mikoa ya Morogoro, Iringa, Mbeya na nchi jirani ya Zambia. 

Bila kutarajia Dk. Mwakyembe alifika katika stesheni hizo saa mbili na nusu usiku, ikiwa ni punde tu baada ya kurejea kutoka katika safari ya kikazi nje ya nchi na uvamizi wake ulizaa matunda baada ya treni hiyo iliyokuwa iondoke Dar es Salaam saa saba mchana kufanikiwa kuondoka saa sita usiku wa kuamkia jana. 

Jitihada za Waziri Mwakyembe, zilileta matumaini mapya baada ya jitihada za uongozi wa TAZARA kugonga mwamba kwa kile kinachodaiwa ni kushindwa kumudu ununuzi wa mafuta ya treni (dizeli) kutokana na kukosa fedha. 

Hatua hiyo inadaiwa kutokana na kampuni za mafuta zilizokuwa zikiiuzia dizeli mamlaka hiyo kusitisha huduma hiyo hadi pale TAZARA itakapolipa malimbikizo ya madeni. 

Mgomo huo uliifanya TAZARA kufanya makubaliano na kampuni ya Lake Oil inayotoa huduma hiyo hivi sasa, ingawa nayo imetoa sharti gumu la kulipwa fedha taslimu ndio itoe mafuta. 

Hali hiyo tete inaelezwa kuzifanya safari za abiria wa TAZARA zinazopaswa kufanyika Jumanne na Ijumaa kuwa za kubahatisha na zisizozingatia muda, kitendo kilichomfanya Waziri Mwakyembe atoboe siri kuwa uongozi wa juu wa mamlaka hiyo unahujumu safari hizo, na si uhaba wa fedha wala dizeli. 

Alitoa maneno hayo juzi usiku baada ya kuwaokoa abiria zaidi ya 1,000 waliokuwa wamekwama katika stesheni hiyo wakisubiri kusafiri na treni hiyo katika vituo tofauti 65 vilivyopo kati ya Dar es Salaam na New Kapiri Mposhi. 

No comments:

Post a Comment