Jessca Nangawe
MABINGWA wa soka nchini, Simba wameshinda vita ya kumwania winga wa Azam FC, Mrisho Ngasa, na sasa nyota huyo anatarajia kuvaa kwa mara ya kwanza jezi za rangi nyekundu na nyeupe msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.Ngasa aliyekuwa pia akiwania na klabu yake iliyompa chati, mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga ya Dar es Salaam, amejiunga na Wekundu hao wa Msimbazi kwa mkopo.
Awali ilitegemewa kuwa, Ngasa aliyechoka kuendelea kukosa namba kikosi cha kwanza cha Uwanja wa Chamazi, angejiunga na timu yake ya zamani ya Yanga.
Azam ilitangaza kupitia tovuti yao mwanzoni mwa wiki hii, kwamba iko tayari kumuuza Ngasa kwa timu yoyote itakayofika dau la dola 50,000.
Taarifa hiyo ya kwenye tovuti ilikuja siku chache tangu Ngasa aonekana akiibusu nembo ya klabu ya Yanga wakati akishangilia bao kwenye mechi ya Kombe Kagame.
Katika ofa yao, Yanga ilisema ingekuwa tayari kumtwaa mchezaji huyo kwa dau la Sh20 milioni, huku wapinzani wao Simba wakija na dau la Sh25 milioni.
Lakini mwenyewe Ngasa alipoulizwa kuhusu kupelekwa kwa mkopo Simba, alionekana kushangazwa na habari hizo na kusema hafahamu lolote.
"Na mimi nimesikia watu wanasema kwamba natakiwa kwenda Simba kwa mkopo. Naloweza kukuambia ni kwamba, mimi naheshimu mkataba wangu," alisema Ngasa.
"Sijaambiwa lolote na viongozi wangu, kwa maana hiyo basi mimi bado mchezaji halali wa Azam mpaka itakapotangazwa tofauti."
Meneja wa Azam, Patrick Kahemela aliithibitishia Mwananchi jana kuwa, klabu yao imeamua kumpeleka kwa mkopo Ngasa klabu ya Simba.
"Kwa sasa bado ana mkataba na Azam, tumeamua kumtoa kwa mkopo kwenda Simba mpaka mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu," alisema Kahemela.
Kahemela alisema ameshangazwa na hatua ya Yanga kushindwa kufika kwenye mazungumzo ya kumsajili mchezaji huyo kama walivyokuwa wamepanga.
"Yanga walikuwa wa kwanza kuleta ofa yao, na sisi tuliwapa wao zaidi nafasi kuliko Simba, lakini walipopaswa kuja kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho hawakutokea," alisema.
Aliongeza: "Yanga walifanya mzaha katika suala hili. Tulimtafuta Katibu Mkuu [Mwesigwa Celestine] lakini hakuonyesha kujali."
Taarifa za Ngasa kutua kwa mkopo Simba pia zilithibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange.
"Tumemalizana na Azam kuhusu suala la Ngasa. Huyu sasa ni mchezaji wetu, atasaidia kuimarisha safu ya ushambuliaji," alisema Kaburu.
No comments:
Post a Comment