Hii ni wiki ya mwisho kwa wabunge wetu kuendelea kuishi mjini Dodoma ambako tangu Aprili wamepiga kambi wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya wizara mbalimbali za Serikali ikiwa ni mara ya kwanza kwa mfumo huo kuanza kutumika nchini.
Wengi tulizoea kuiona Dodoma ‘ikiwaka moto’ kuanzia wiki ya pili ya Juni hadi Agosti ambako mipango na makusudio ya Serikali viliwasilishwa bungeni, wakati ule tukianza na bajeti kuu ya Serikali na kufuatiwa na mipango ya wizara.
Ni muda mrefu kwa wawakilishi wetu wengi ambao wamekuwa wakiishi mbali na familia zao, huku baadhi wakiwa wameacha mbali wake, waume au rafiki zao wa kike na kiume.
Kama Waswahili wasemavyo, mgeni njoo mwenyeji apone, wachuuzi wa Dodoma na wamiliki wa nyumba za kupanga, zile za wageni, mama lishe, wenye baa na grosari walikuwa katika kipindi kizuri cha mavuno.
Ni mambo mengi mno yamesemwa kuhusu mienendo ya baadhi ya wabunge wetu wakiwa mjini Dodoma ambako kuna baadhi ya dada au binti zetu kutoka mikoa mbalimbali wakiwamo hata wasomi wa vyuo vikuu vya umma na binafsi ambao wamekuwa sehemu ya huduma, burudani kwa wawakilishi wetu, wengi wakijipitisha mbele yao watunga sheria usiku na mchana, wakisaka soko, ofa mbalimbali.
Mambo mengi ya msingi na yenye masilahi kwa nchi yetu na watu wake yamejadiliwa kwa kina kuhusu mpango wa Serikali hasa wa kuwatumikia ipasavyo Watanzania kwa lengo la kutimiza ahadi lukuki ambazo ilizitoa mwaka 2010 pale ilipoomba ridhaa ya wananchi ili kuingia madarakani.
Tumewasikia wabunge, tumewaona wengine laivu kupitia runinga au vyombo vingine vya habari wakati wote walipokuwa kazini mjini humo kwa miezi karibu miwili.
Hata hivyo, inashangaza kuona kuwa wapo wengine ambao kwa siku zote wamekuwa bubu, hawakusema au hata kufungua vinywa vyao kuchangia au kujadili mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiendelea mbele yao.
Watanzania, katika baadhi ya nyakati tumeshudia jinsi ambavyo ukumbi wa kisasa wa Bunge kule Dodoma ambao mwanzo wa mwaka tuliambiwa na wabunge kuwa ulikuwa unavuja sehemu ya paa lake.
Hali hiyo ilitishia maisha yao na hasa ulivyokuwa mtupu, viti vingi havina wabunge, jambo ambalo kwa hakika lilinishangaza mimi na wengine.
Ninakumbuka wakati mmoja niliwahi kuandika hapa nikiomba ruhusa isiyo rasmi kutoka kwa Spika Anne Makinda, kwanza niingie au hata kukanyaga zulia jekundu na bluu ukumbini humo.
Hapo nilitaka nini, hakuna shaka nilitaka nikachukue viti vile vyote vitupu na meza na kisha kuwapelekea maelfu ya watoto wetu si wanafunzi wote na walimu kote nchini au katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ambao hawajui utamu wa kukalia kiti darasani.
No comments:
Post a Comment