Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa yeyote ambaye atajaribu kuchezea usalama na mipaka ya Tanzania atakiona cha mtema kuni.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liko imara tayari kulinda mipaka ya Tanzania wakati wowote na saa yoyote.
Rais Kikwete ametoa ujumbe huo mzito leo, Alhamisi, Julai 25, 2013, wakati alipozungumza na wananchi wakati Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kwenye Kambi la JWTZ ya Kaboya, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera.
Mara baada ya kushuhudia sherehe za kumbukumbu hizo ambako miongoni mwa mambo mengine ametembelea makaburi ya askari wa Tanzania waliopoteza maisha yao wakati wa kuikomboa nchi kutokana na uvamizi wa Idi Amin wa Uganda na kuona silaha zilizotumika katika vita hivyo vya 1978/79, Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo:
“Laleni usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani kwa sababu Jeshi letu liko imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu kuivamia ama kuichokoza nchi yetu atakiona cha mtema kuni. Nchi iko salama na Jeshi liko imara kulinda nchi yetu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ujumbe wetu mkubwa wa leo ni kwamba tuko tayari wakati wote na, saa yeyote kuilinda nchi yetu na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine. Hivyo, kamwe hatuwezi kumruhusu yeyote kuicheza nchi yetu, ama kuichezea ama kuimega nchi hii. Kama tulivyoshughulika na Amin naye tutashughulika naye vivyo hivyo.”
Rais Kikwete amesema kuwa shughuli ya kulinda amani ni ghali mno:“Na moja ya gharama hizo ni makaburi haya ya ndugu zetu ambao wamelala hapa baada ya kupoteza maisha yao katika vita dhidi ya Nduli Idi Amin. Tutaendelea kuwaenzi kwa sababu hawa walijitolea maisha yao kulinda mipaka ya nchi yetu, kulinda amani ya nchi yetu na usalama wake na wetu sote.” Kiasi cha askari 619 waliopoteza maisha yao wamelazwa kwenye makaburi hayo ya Kaboya.
Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake kwa ushauri wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania inaangalia jinsi gani ya kuwahudumia vizuri zaidi askari wa Tanzania ambao walipata vilema katika vita hivyo na bado wanaendelea kuishi.
“Nimesikia kuna malalamiko lalamiko kuhusu ubora wa jinsi tunavyowahudumia na hivyo tutazungumza na Jeshi kuhusu njia bora zaidi ya jinsi ya kuwahudumia. Hawa ni mashujaa wetu, ni watu waliojitolea maisha yao kuweza kulinda uhuru wetu. Tunaendelea kuwashukuru na kuwaenzi. Hii ndiyo sababu sherehe za leo ni sherehe kubwa kwa nchi yetu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
25 Julai, 2013
No comments:
Post a Comment