BREAKING NEWS
JESHI la Polisi mkoani Kagera linamshikilia mwanaume mmoja kwa tuhuma za kushiriki katika tukio kumvamia na kumkata mapanga albino kwa lengo la kumuua na kuchukua viungo vyake.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Andrew Salewi alidai kuwa tukio hilo lilitokea JANA , ambapo kundi la watu waliokuwa na silaha za jadi walivamia na kuvunja nyumba alimokuwa akiishi albino huyo, Miriam Stanford (28), mkazi wa Kata ya Nyamiaga wilayani
Ngara saa 7.00 usiku na kuanza kumkata kwa mapanga.
Hata hivyo wavamizi hao hawakufanikiwa kumuua huyo baada ya albino kupiga kelele za kuomba msaada kwa majirani, lakini walimkata na kisha kukimbia na mkono wake wa kulia.
Kamanda Salewi alisema kukamatwa kwa mtu huyo kulitokana na mtuhumiwa kutambuliwa na kutajwa na albino huyo kuwa ni miongoni mwa watu waliomvamia siku
hiyo.
Kamanda Salewi jeshi lake linawahoji watu wanne ambao ni jamaa wa albino huyo walikuwa wakiishi naye katika nyumba hiyo ili kujua kwa nini walishindwa kutoa msaada wa haraka kwa ngudu yao.
Alifahamisha kuwa kabla ya wavamizi hao kuondoka walitaka kumkata mkono wa pili, lakini walishindwa kutokana na kelele za kuomba msaada zilizokuwa zinapigwa na albino huyo na majirani kuanza kukusanyika kwa ajili ya kumsaidia.
Baada ya tukio hilo, albino huyo alipelekwa katika hospitali teule ya Murgwanza iliyoko wilayani Ngara ambako amelazwa kwa matatibabu kutokana na majeraha aliyopata baada ya kukatwa mkono wa kulia.
Kamanda huyo alidai kuwa kinachoshangaza ni kwamba albino huyo alikuwa akiishi na watu wanne ambao hakuwataja majina yao wakati wa tukio walikuwa ndani ya nyumba hiyo lakini hawakumsadia.
Jeshi hilo limetoa onyo kwa watu wanaojihusisha na matukio ya kuwajeruhi na kuwaua watu hao wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za kishirikina na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
No comments:
Post a Comment