.
.
Friday, October 03, 2008
WASABATO WANGOJEA KUJA ULAYA
KIKUNDI cha waumini wa dhehebu la Waadiventista wa Sabato kinachojiita Masalia ambao wameweka kambi chini ya mti katika bonde la Mto Msimbazi, sasa kinaonekana kuanza kuzidiwa; baadhi yao wanaonekana kudhoofika kiafya.
Waumini hao, ambao wamekuwa na msimamo na imani zisizotetereka, wanaamini kuwa siku moja watafunguliwa njia na kwenda kuhubiri barani Ulaya bila ya kutumia tiketi, visa za nchi wala hati za kusafiria licha ya majaribio yao matatu kuisha kwa kutimuliwa kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mwalimu Julis K. Nyerere.
Lakini sasa wanaonekana kupoteza kilo mwilini huku nuru ikianza kutoweka kwenye nyuso zao.
Wakizungumza kwenye kambi yao jana, waumini hao walisema hali hiyo inasababishwa na imani yao.
“Sisi hatuumwi kabisa, bali haya ni mambo ya imani," alisema mmoja wao, ambaye aliomba jina lake lisitajwe. "Ni imani hiyo ndio inatufanya tuendelee kuwepo mahali hapa.”
Alisema hata wakati wakiwa wadogo waliambiwa kuwa hawataweza kula nyama ya kanga kwani wakila wangeugua, na kurithisha imani yao kwa watoto na hadi leo hawali.
“Sasa kwa mfano huo unaweza kuona ni jinsi gani imani inavyoweza kumbadilisha mtu, pia imani hiyo hiyo inaweza kumfanya mtu akaugua,” alisema muumini huyo
Aliongeza kusema: "Watu wengi wanatushangaa kutoka na imani yetu kwa kuwa si rahisi kwa mtu wa kawaida kulala au kuishi mahali kama hapa tunapoishi sisi.
"Lakini sisi tumewekewa ngao na Mwana wa Mbinguni. Tunakula hapa na tunalala hapa, lakini hakuna magonjwa yatakayotupata."
“Bwana katuwekea ngao hakuna magonjwa wala malaria hapa,unajua mwanadamu alipomwacha mungu ndipo tabu ilipoanza”alisema muuni huyo
Waumini hao, ambao idadi yao inaonekana kuanza kupungua, wanaendelea kuishi chini ya mti wa mwembe katika bonde hilo huku wakiendelea na imani yao kuwa siku moja wataenda nje kuhubiri injili.
Lakini waliiambia Mwananchi kuwa idadi yao haijapungua na wanachosubiri ni amri ya kwenda huko waendako.
“Safari bado ipo, tunasubiri Mungu akisema, tutaondoka,” alisema muumini mwingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment