.

.

.

.

Saturday, November 01, 2008

MGAO WA MAPATO UCHUNGUZWE

JUZI Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lilitangaza mapato ya mechi ya Simba na Yanga iliyofanyika Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo kiasi cha sh.239,829,000 kilipatikana. Hatuna tatizo na fedha zilizopatikana, lakini kilichotushangaza ni fedha hizo zilivyogawanywa kwa watu mbalimbali baada ya mchezo huo, ambao wana haki ya kupata kulingana na utaratibu uliowekwa. Imetushangaza zaidi kukuta timu ambao ndio wadau wakubwa zikigawana sh. milioni 41 kila moja, huku mgawo wa uwanja ukiwa sh.milioni 43. Wala haihitaji nguvu za ziada kujua kuwa timu zinaingia gharama kubwa kwa ajili ya mchezo, lakini zinapozidiwa mgawo na uwanja au zinapotofautiana kidogo na TFF ni jambo linalokatisha tamaa sana. Katika mgawo uliotangazwa juzi sh.43,358,948 zililipia uwanja, Simba na Yanga kila moja ilipata sh.41, 191,000, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), lilipata sh. 2,167,947, TFF sh. 21, 679,474, Mfuko wa Maendeleo ya Michezo (FDF), sh. 19,511, 526 na sh. 4,335,894 ziligawiwa kwa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA). Kuna haja kwa wadau kukaa chini na kutazama fedha zinazoenda BMT, Mfuko wa Maendeleo na hata vyama vya michezo, ni kubwa sana na zinaziumiza klabu pamoja na wachezaji kwa ujumla. Hatupingi zisipewe mgawo, lakini tunasema kuwe na kiwango ambacho hakiwezi kuziumiza klabu, maana kwa makato haya ni kuzitwisha mzigo klabu zetu. Tunasema kama uwanja unapata fedha nyingi kuliko klabu, huku TFF ambayo nayo ina wadhamini na haina mchezaji hata mmoja inachukua zaidi ya nusu ya fedha inazopata klabu, au DRFA na wengine wengi wanapewa, tunajenga klabu za namna gani? Tukubali kufanya mabadiliko katika mgawo, ili angalu tuzisaidie klabu zetu ambazo zina majukumu mengi mazito katika kuziandaa timu zao na si kama tunavyofanya sasa.

No comments:

Post a Comment