.

.

.

.

Wednesday, November 05, 2008

MTOTO YATIMA ACHUNWA NGOZI

MTOTO yatima ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Kilolo mkoani Iringa, Johansi Mlosa (11), amekutwa ameuawa na watu wasiofahamika na mwili wake kuchunwa ngozi huku baadhi ya viungo vikinyofolewa. Johansi ambaye alitoweka kwa zaidi ya wiki moja sasa, mwili wake ulikutwa umetupwa katika Mto Mtitu, umbali wa meta 100 kutoka eneo wanaloishi mabuluda wa Kanisa Katoliki ukiwa na dalili za kukauka. Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, babu wa marehemu, Bw. Johnson Mlossa (56) na binamu wa marehemu, Bw. Alex Matinya (29) walidai kuwa mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha Oktoba 13 mwaka huu saa 11 jioni baada ya kutoka shuleni. Bw. Mlossa alisema mtoto huyo alikuwa akiishi katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Misheni kutokana na baba na mama yake kufariki dunia Juni 6, 2003. “Kutokana na uwezo wangu mdogo wa kumtunza mjukuu wangu, nilifikisha maombi yangu kwa viongozi wa kituo na wakanikubalia kusaidia kumtunza mjukuu wangu kituoni na kumwendeleza kielimu,” alisema babu huyo. Kutokana na msaada mkubwa wa kituo hicho ambao walikuwa wakiutoa kwa mjukuu wake, hakuweza kurudi nyumbani na badala yake alikuwa akishinda na watoto wenzake kituoni. Hata hivyo, alisema akiwa katika shughuli zake za kila siku, alifuatwa na mmoja kati ya walezi wa kituo hicho, ambaye alitaka kujua kama mtoto huyo amerudi nyumbani kwa siku hiyo. “Nilifuatwa na mlezi wa kituo hicho ambaye aliniuliza kama mjukuu wangu alirudi nyumbani baada ya kutoonekana kituoni jioni ambayo ilikuwa si kawaida yake kuchelewa kurudi,” alisema. Alisema kutokana na taarifa hiyo, ndipo jitihada za kumtafuta zilipoanza kwa usiku huo na siku iliyofuata na kulazimika kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Mtitu, kuhusu kupotea kwa mtoto huyo katika mazingira hayo. Bw. Mlossa alidai kuwa baada ya ukimya kuendelea kwa siku mbili, alilazimika kwenda kutangaza katika kituo cha Radio Country FM mjini hapa, ili kuwaomba wasamaria wema watakaomwona kutoa taarifa Polisi au kwa ndugu. "Nafikiri baada ya matangazo hayo kutangazwa mara kwa mara wauaji waliamua kuutoa mwili huo mafichoni na kuuweka jirani na eneo hilo la kituo, ili watu waweze kuuona kirahisi zaidi, kwani tumeshangaa kuuona jirani hapa wakati watu wamekuwa wakipita kila siku katika eneo hilo bila kuuona,” alisema. Aliongeza kuwa mtoto huyo alionekana Oktoba 26 mwaka huu akiwa amechunwa ngozi na mazingira yalionesha kuwa wauaji kabla ya kumuua, alitekwa na kwenda naye mbali na eneo la kituo na kumuua. Bw. Mlossa alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ukiwa mtoni, lakini cha kushangaza ulikuwa umekauka kama uliokuwa umeanikwa juani kwa muda mrefu. “Hata kama ni kipofu hawezi amini, kwani kama kweli mtoto huyo alikuwa amekufa maji, mwili wake ungeonesha dalili za mtu aliyekufa maji hata kutoa harufu na kuvimba,” alisema. Alitaja baadhi ya viungo vilivyonyofolewa mbali na kuchunwa ngozi kuwa ni sikio la kulia, sehemu za siri, vidole vitatu vya mkono wa kulia na vitatu vya mguu wa kulia na sehemu ya ziwa la kulia. Kwa upande wake, Bw. Matinya alisema bado hajafahamu malengo ya wauaji, kwani mauaji ambayo amekuwa akiyasikia zaidi ni ya albino na hata hivyo katika wilaya hiyo hajapata kuyasikia. Bw. Matinya alisema anachofahamu ni kuwa binamu yake huyo hakuwa mlemavu wa aina yoyote zaidi ya kuwa na uwezo mkubwa darasani katika masomo. Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Dkt. Athuman Mfutakamba, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba anajiandaa kuitisha mikutano ya hadhara na wananchi kwa ajili kukemea vitendo hivyo vinavyofanywa katika wilaya hiyo. Alisema pamoja na kuwa uchunguzi wa mauaji hayo unafanywa na Polisi, inaonesha kuwa mauaji hayo yanahusiana moja kwa moja na imani za kishirikiana. Aliwataka waganga wa kienyeji wanaodanganya wananchi kwa kuwataka wapeleke viungo vya binadamu kuacha mara moja au kuhama katika wilaya hiyo kabla ya kubainika. Hayo ni mauaji ya pili kutokea katika wilaya ya Kilolo mwaka huu, ambapo mauwji kama hayo yalimkuta mwanamke ambaye alichinjwa na kuondolewa baadhi ya viungo na mwili wake kukutwa umefungwa katika mfuko wa sandarusi na kufichwa kichakani. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Bw. Advocate Nyombi, alisema Jeshi lake lina taarifa ya kupotea kwa mtoto huyo na kukutwa amekufa, ila bado haliwezi kuthibitisha kama alichunwa ngozi na kutolewa baadhi ya viungo kutokana na mwili huo kukutwa majini,

No comments:

Post a Comment