HISTORIA inaweza kuandikwa leo nchini hapa na ndoto ya hayati Dkt. Martin Luther King, inaweza kuwa kweli iwapo mamilioni ya Wamarekani wanaojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa kihistoria, wataamua kumchagua mwanasheria, mwenye asili ya Kenya na visiwa vya Zanzibar, kuwa Rais wa 44 wa nchi hiyo na kupuuza vitisho, fitna na mizengwe iliyoanza kujitokeza. Wakati uchaguzi huo ukifanyika leo, tayari kumeanza kuripotiwa vitendo vya fitina lengo likiwa la wazi-kuwafanya baadhi ya watu wasijitokeze kupiga kura hususani miongoni mwa jamii za Wamarekani weusi. Kutumiwa barua pepe zinazochanganya, kukuta mabango nje ya nyumba yanayoeleza habari tofauti na zisizo sahihi kuhusu uchaguzi na kupigiwa simu za kushawishi, ni miongoni mwa mambo ambayo ni kawaida katika uchaguzi wa Marekani. Lakini safari hii, huku ikiaminika kuwa huenda Obama, Mmarekani mwenye mchanganyiko wa weusi na uzungu huenda akashinda, kama kura nyingi za maoni zilivyoonesha, kumekuwa na matukio ya watu weusi kulengwa zaidi na vitisho na fitna hizo. Katika maeneo mengi yenye wakazi wengi wenye asili ya Afrika hasa karibu au ndani ya mji wa Philadelphia, kumekuwa na matangazo mengi yenye kuwaonya watu kuwa wanaweza kukamatwa iwapo itabainika kuwa huko nyuma waliwahi kukutwa na hatia ya kosa lolote la jinai au hata kuwahi kuegesha gari bila kuwa na tiketi maalumu katika maeneo yaliyotengwa. Wamarekani weusi kwa kawaida wanahusika katika makosa mengi Marekani, ingawa sheria za uchaguzi nazo hazimzuii mtu kupiga kura kwa sababu ya makosa yake ya nyuma kama taarifa hizo zinavyopotosha. Mjini Virginia, kumekuwa na mabango ya kitapeli yenye mhuri na nembo za Jumuiya ya Madola ambazo zimebainika kutaka kuwalaghai wafuasi wa chama cha Democrat cha Bw. Obama, ili wasijitokeze leo kupiga kura. Matangazo hayo yamekuwa yakisema kuwa kutokana na wingi wa wapiga kura, uchaguzi huo umepangwa kufanyika siku mbili-leo kwa ajili ya wapiga kura wa Republican cha Bw. John McCain na kesho kwa ajili ya wapigakura wa Democrat. Fitna kama hizo zimesababisha mjini wanawake wawili wenye asili ya Kispaniola kufungua kesi wakilalamika kusumbuliwa na mwendesha mashitaka aliyekuwa akiwafuatafuata na kuwatisha kuwa angewaita maofisa wa Uhamiaji iwapo wangekwenda kupiga kura hata kama tayari wao ni raia wa Marekani. Mwendesha mashitaka huyo anadaiwa kuwa wa chama cha Republican. Mjini Pennsylvania, ilinaswa baruapepe maarufu inayojaribu kumnasabisha Bw. Obama na mauaji ya Wayahudi na kuwashawishi Wayahudi wenye uraia wa Marekani kutomchagua mgombea huyo. Vitisho hivyo vimekuja wakati ambapo pamoja na Obama kupewa nafasi kubwa ya kushindwa, ikiwa imebainika pia kwamba miongoni mwa wapiga kura wengi wapya waliojiandikisha, wengi wao ni wafuasi wake.Zanzibar na Obama
Pamoja na utafiti mwingi wa kihistoria kukubaliana katika jambo moja kuwa Barack Hussein Obama ni Mmarekani mwenye asili ya Kenya alikozaliwa baba yake mzazi, lakini visiwa vya Zanzibar navyo, vina nasaba na mgombea huyo, umeendelea kubaini utafiti wa Majira. Wakati nchini Kenya ndiko alikozaliwa baba yake Obama, ni visiwani Zanzibar ambako babu yake mzaa baba, Mzee Onyango alikoishi, kuoa na hata kusilimishwa na kuwa Mwislamu. Mzee Onyango aliyekuwa mpishi enzi za utawala wa kikoloni, alikwenda kuishi Zanzibar baada ya kuwatumikia Waingereza kwenye vita za Dunia na ndiko alikosilimu na hata kuchukua jina la Hussein ambalo kwa sasa ni jina rasmi la pili la Obama anayeitwa Barack Hussein Obama. Obama ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Columbia alikosoma Uhusiano wa Kimataifa na baadaye kwenda Chuo Kikuu mashuhuri cha Harvard alikochukua taaluma ya sheria, amekuwa mhadhiri kwenye Chuo Kikuu cha Chicago kwa miaka 20 na ni wakili wa kujitegemea, aliyebobea katika sheria za Katiba na haki za kiraia.
Source: Gazeti la majira
No comments:
Post a Comment