
Serikali imesema inafanyia uchunguzi madai ya kutishiwa kuuawa yaliyotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, na itachukua hatua kali endapo itabaini kuna ukweli. Akizungumza jana katika kipindi cha Jambo Afrika cha TBC, Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha, alisema serikali inachunguza waliohusishwa na tuhuma hizo na wakibainika watachukuliwa hatua. Masha alisema kwa kuwa Mengi alisema ana ushahidi wa tuhuma alizotoa, serikali haitapata shida ya kuhangaika na ushahidi na imemtaka apeleke ushahidi huo. Alisema tayari ameshaagiza maofisa wa wizara yake walifanyie uchunguzi wa kina suala hilo na kisha wampe taarifa. Waziri Masha alisema ni jukumu lake kuhakikisha usalama wa raia na mali zao hivyo hawezi kuacha kufanyia kazi suala zito kama hilo. ``Mengi alisema ana ushahidi wa kutosha hivyo tumempa siku saba atuletee huo ushahidi ili tuufanyie kazi na ikibainika kuna ukweli hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika,`` alisema Waziri Masha. Kwa mujibu wa Masha, endapo Mengi hataleta ushahidi wa kuthibitisha tuhuma alizotoa serikali itaangalia hatua za kuchukua. Kwa upande wake,
Mengi alisema jana kuwa siku saba alizopewa na Masha ni nyingi sana na kuongeza kuwa angempa muda kidogo ili auwasilishe ushahidi huo kwa kuwa yu tayari hata leo hii (jana). Alisema amemshangaa waziri huyo kama alizungumza kama msemaji wa wizara hiyo ama msemaji wa mawaziri vijana kwa kuwa yeye (Mengi), alichozungumzia ni serikali nzima kwa kuwa wizara nyingi zina mawaziri vijana. ``Wizara ya Masha inatoa hoja nyingi. Kuna wengine wanasema nimeripoti taarifa za vitisho polisi na wengine wanasema sikuripoti,`` alisema Mengi na kuongeza kuwa, kama itabainika amedanganya, atakuwa tayari kufungwa na kama ni kweli Masha awe tayari kujiuzulu.
Katikati ya wiki hii, Reginald Mengi alimtuhumu Waziri mmoja kuwa ameagiza abambikiwe kodi bandia ya kiasi kikubwa atakachoshindwa kulipa ili hatimaye afilisiwe. Alimtuhumu waziri huyo kuwa amekuwa akimtumia ujumbe wa vitisho kutokana na vyombo vyake vya habari kuwa mstari wa mbele katika kupigia kelele ufisadi. Mengi alisema waziri huyo ameahidi kumnyamazisha kabisa kutokana na kupigia kelele vitendo vya ufisadi. Mengi alisema waziri huyo amekuwa akijigamba kuwa atamnyamazisha kwa kuhakikisha anafilisiwa kama alivyofilisiwa tajiri mmoja nchini Urusi. Mengi alisema kuwa waziri huyo anadai kuwa vyombo vyake vya habari vimekuwa mstari wa mbele kupiga vita ufisadi, jambo ambalo kwa maoni yake siyo zuri na linawanyanyasa baadhi ya watu. ``Nilitarajia waziri huyo msomi sana angefahamu jinsi vyombo vya habari vinavyofanyakazi...anayeamua nini kiandikwe na nini kisiandikwe ni mhariri wa gazeti ambaye taaluma yake ni uandishi wa habari na si mmiliki,``alisema. Alisema ingawa tayari amemsamehe waziri huyo, lakini anapaswa kujua kuwa asiyekemea maovu katika jamii anakuwa sehemu ya maovu hayo.
Mengi alisema waziri huyo na wale ambao wamekuwa wakimtumia ujumbe wa vitisho lazima wakumbuke kuwa hata wakifanikiwa kumnyamazisha yeye (Mengi), moto wa kupiga vita ufisadi uliokwishawashwa katika akili za Watanzania hauwezi kuzimika kamwe.
Alisema lazima ieleweke kuwa sauti za maskini na wanyonge katika jamii hazisikiki kwa urahisi na vyombo vya habari ndivyo vimechukua jukumu la kusaidia kupaza sauti zao. Mengi alisema ni wajibu wa kila mtu aliye na uwezo wa kusema kwa sauti kubwa kwa niaba ya wanyonge na maskini ili kutokomeza ufisadi. ``Nampongeza sana Rais Jakaya Kikwete kwa kuguswa na sauti na vilio vya wanyonge na maskini wa Tanzania kuhusu ufisadi na hatua za kijasiri zinazochukuliwa na serikali yake dhidi ya ufisadi....sisi sote lazima tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu azidi kumpa ujasiri, nguvu na hekima nyingi wakati huu wa majaribu makubwa,`` alisema Mengi. Alisema ufisadi wote ambao Rais Kikwete amekuwa akipambana nao ulifanyika wakati wa serikali ya awamu ya tatu. Alisema Kikwete amekuwa jasiri na shupavu katika kupambana na maovu ambayo alikuta tayari yamefanyika wakati anaingia madarakani. Mengi aliwashauri waandishi wa habari kuandika pia mambo mema yanayofanywa na serikali ya awamu ya nne, badala ya kuelemea zaidi katika ufisadi. ``Tuendelee kuandika habari za ufisadi lakini mazuri yanayofanywa na Rais Kikwete nayo yapate nafasi ili isije ikaonekana kama hajafanya kitu wakati yapo mengi sana amefanya kwa kipindi hiki kifupi alichokaa madarakani,`` alisema. Vile vile, Mengi alisema kuna watu wameanza kutoa vitisho dhidi ya watu wanaopinga vitendo vya ufisadi. Alisema watu hao wamebuni mbinu mbalimbali za kukwamisha wale ambao wamekuwa mstari wa mbele kupambana na vitendo hivyo. ``Wakati kuna kundi la watu limeamua kwa dhati kabisa kupambana na ufisadi, kundi lingine limeamua kupingana nao lakini nawapa moyo kuwa wasitishike na wasikate tamaa, wazidi kupambana na waamini kuwa ushindi ni wao,`` alisemakwenye simu yake kutoka kwenye simu namba. Baadhi ya ujumbe wa vitisho aliotumiwa 0768 373967 ulisomeka hivi: ``Ni afadhali kunyofoa roho yako ipotee kuliko uendelee kuchafua amani na utulivu wa nchi kwa tamaa zako za kuutaka urais...ugomvi wako na Manji hauwezi kutufanya watu wote tuingie katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, uliyofanya yanatosha enough is enough kaa tayari.``
Ujumbe wa pili aliotumiwa Mengi ulisomeka hivi : ``Unachafua sana amani ya nchi kwa uchochezi wako unapenyeza sumu ya uzandiki watu waichukie serikali. Hivi ikitokea vita wewe utasalimika? Wewe ni mnafiki mkubwa unajifanya uko karibu na serikali kumbe ni mnafiki wa kutisha jihadhari lazima tutakumaliza.``
No comments:
Post a Comment