.

.

.

.

Sunday, January 18, 2009

KAGODA KUSHITAKIWA YAGEUKA NDOTO YA ALINACHA

NDOTO za Watanzania kuona Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd iliyochota kiasi cha sh bilioni 40 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaendelea kufifia baada ya kubainika kuwa serikali haina ushahidi wa kutosha kuiburuza mahakamani.
Kukosekana kwa ushahidi huo kunaelezwa ni mipango madhubuti iliyoandaliwa na baadhi ya viongozi waliopo na waliondoka serikalini kwa kushirikiana na wafanyabiashara maarufu kupoteza nyaraka zote ambazo zingesaidia kampuni hiyo kufikishwa mahakamani kama walivyofikishwa baadhi ya watuhumiwa wengine waliochota fedha kwenye akaunti hiyo.
Pamoja na Rais Jakaya Kikwete, kukabidhi mafaili ya watuhumiwa wote wa wizi wa EPA kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi, miezi miwili iyopita, ofisi yake imeshindwa kupata ushahidi wa kutosha kuishtaki Kagoda kama iliyotarajiwa na wengi.
Kampuni hiyo ambayo umiliki wake unahusishwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) inadaiwa walichota fedha hizo kwa ajili ya kusaidia kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ambao CCM iliibuka na ushindi wa kishindo.
Chanzo cha habari kutoka ofisi ya DPP, kiliiambia Tanzania Daima Jumapili, kuwa wamiliki wa Kagoda walijua nini kitatokea baada ya wizi huo, hivyo kwa kushirikiana na viongozi walifanya kila njia kuhakikisha hawaachi nyaraka zozote ambazo zingekuja kuwaleta matatizo siku za usoni.
Miongoni mwa mbinu zilizotajwa kutumiwa na wahusika hao ni kwenda benki na kunyofoa nyaraka zote zilizokuwa zikionyesha mtu na akaunti ambayo fedha hizo ziliingia, nyaraka za umiliki wa kampuni katika Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (Brella) nazo mpaka sasa hazijulikani zilipo.
Chanzo hicho kimeongeza baada ya kelele za ufisadi kuzidi hapa nchini na Kampuni ya Kagoda kuandamwa, wamiliki halisi walianza kujawa na hofu ya kutajwa hivyo wakaamua kuwaendea baadhi ya viongozi na kutoa tishio kuwa kama hawatalindwa katika kashfa hiyo basi watakuwa radhi kuueleza umma walivyoshirikishwa katika wizi huo.
Kutokana na tishio hilo, baadhi ya viongozi waliopo serikalini na wale waliomaliza muda wao waliwahakikishia wamiliki hao kuwa kamwe hawataguswa kwa kuwa kampuni hiyo imebeba siri nzito ambayo ikiwekwa hadharani taifa litatikisika.
“Wamiliki wa Kagoda wanajulikana lakini serikali haiwezi kuwakamata kwa kuwa hakuna ushahidi lakini pia wana siri nzito, ndiyo maana wizi wa nyaraka ulifanyika kwa kiwango cha juu,” kilidokeza chanzo chetu.

No comments:

Post a Comment