TANZANIA iko hatarini kuathirika kiuchumi kama meli za mizigo kutoka nje ya nchi, zitapunguza safari zake nchini kwa hofu ya kuvamiawa na maharamia wa Kisomali, katika Pwani ya Aden.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema vitendo vya uharamia katika Bahari ya Aden, vinatokana na kuanguka kwa dola ya Somalia na vinadhaminiwa na baadhi ya matajiri wa Dubai.
Alisema, tatizo hilo nin kubwa na kwamba, hata kama manuari za kivita za dunia nzima zikipiga doria katika bahara hiyo, hatamudu kutatua tatizo hilo.
Alisema hiyo inatokana na ukubwa wa Bahari ya Somali ambayo inaingia Kenya na Tanzania.
Dk Bana alisema, kutokana na kukithiri kwa uharamia huo, meli za mizigo zinazokuja Tanzania, zinaweza kupunguza au kusitisha safari zake kwa hofu ya kuvamiwa au baada ya mashirika ya bima ya kimataifa kupandisha bei.
"Ili meli yoyote ya mzigo ifike Tanzania lazima ipitie Bahari ya Somalia, kwa hiyo kama vitendo hivyo vitaendelea basi kuna uwezekano mkubwa wa makampuni ya meli hizo, kusitisha safari zake" alisema Dk Bana.
Kwa mujibu wa maelezo yake, watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, wana silaha za kutosha na zinauzwa kama njugu katika mji wa Mogadishu.
Alisema kampuni zinazoajiri vijana hao, ni za wasomi wakubwa wa mtandao wa kompyuta, satelaiti na wanamgambo wa kivita kutoka katikati ya Somalia.
"Unajua tangu kuanguka kwa dola ya Somalia nchi hiyo haina serikali ya uhakika, serikali yake ni legelege na ovyo isiyo na uwezo wa kufanya lolote katika tatizo hilo nchini mwake" alisema Dk Bana.
Alisema kama tatizo hilo halitapatiwa ufumbuzi wa kudumu, kuna uwezekano mkubwa wa vijana wa Tanzania kukimbilia Somalia na kujiingiza katika kazi hiyo.
"Tusipokuwa na udhibiti wa vijana wetu, tunaweza kujikuta na wao wanaingia katika kazi hiyo kutokana na ugumu wa maisha, kwa sababu wanaona kwenye vyombo vya habari," alisema Dk Bana.
Alisema, suluhu ya kudumu ya tatizo hilo ni kurudishwa kwa utawala wa kidemokrasia nchini Somalia na mamlaka yake kamili.
Alisema hatua hiyo inapaswa kufuatiwa kuwajengea matumaini mapya vijana wa Somalia hasa kiuchumi ikizingatiwa kuwa kiini cha tatizo ni njaa inayosababisha na hali ngumu ya maisha
No comments:
Post a Comment